Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, imeongeza siku mbili zaidi za kuapisha mawakala wa vyama vya siasa watakaosimamia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Wilson Mahera akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema, tume imeongeza muda huo kuanzia leo hadi 23 Oktoba 2020.
“Tume imeamua hivyo baada ya kubaini baadhi ya maeneo kuna changamoto ya kufikika kutokana na jiografia,” amesema Dk. Mahera
Shughuli ya uapishaji mawakala ilikuwa ifanyike kwa siku moja ya leo Jumatano lakini tangu asubuhi katika maeneo mbalimbali, kumekuwapo na taarifa kutoka kwa vyama vya siasa na wagombea kulalamikia mawakala wao kutoapishwa.
Hata hivyo, Dk. Mahera amesema, watakaoapishwa katika kipindi hicho ni yale majina yaliyowasilishwa na vyama yakiwa na majina yenye namba za simu na yaliyopangwa kwa kila wakala atasimamia eneo gani.
Social Plugin