Na Kadama
Malunde – Malunde 1 blog
Jeshi la
Polisi Mkoa wa Shinyanga limesema limejipanga kikamilifu kusimamia zoezi zima la uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika
Oktoba 28,2020 katika hali ya amani na utulivu na kwamba kamwe halitasita
kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu au watu au kikundi chochote chenye nia
ya kuvuruga zoezi la uchaguzi.
Akizungumza
na vyombo vya habari leo Oktoba 26,2020, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga
ACP Debora Magiligimba amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga
kura kwenye vituo vya kupigia kura wakiwa na amani bila kuhofia usalama wao.
“Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limeimarisha doria za magari na pikipiki,doria za miguu pamoja na doria za mbwa. Lakini pia Askari polisi wa kutosha wamepangwa kwenye vituo vyote vya kupigia kura na maeneo mengine ili kuimarisha ulinzi,hivyo wananchi wote wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura kwani amani ipo ya kutosha”,amesema Kamanda Magiligimba.
“Lakini pia
niwaombe wananchi mara baada ya kupiga kura warudi nyumbani kuendelea na
majukumu yao ya kila siku, wasibakie kwenye maeneo ya kupigia kura. Suala la
kulinda kura ni suala la Jeshi la Polisi siyo wananchi”,amesisitiza Kamanda
Magiligimba.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kufuata sheria,kanuni na taratibu za uchaguzi ili kufanikisha zoezi zima la uchaguzi kumalizika kwa amani na utulivu.
Kamanda huyo
wa polisi amewataka wananchi kutoa taarifa mapema za uwepo wa viashiria vya
uvunjivu wa amani katika maeneo yao ili viweze kudhibitiwa mapema na kwamba
jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu au watu au
kikundi chochote chenye nia ya kuvuruga zoezi la uchaguzi.
Social Plugin