Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC SINGIDA AGAWA ZAWADI YA ROZARI KWA VIJANA

 

RC Nchimbi akikabidhi zawadi ya Rozari Takatifu kwa vijana waliohudhuria Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Singida jana.

Mratibu wa Kongamano hilo na Afisa wa Vijana kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Frederick Ndahani akizungumza na vijana wa mkoa huo kabla ya kumkaribisha RC Nchimbi kufungua Kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jana.

Vijana wakishiriki kikamilifu Kongamano hilo.
 


Na Godwin Myovela, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi ametoa zawadi ya Rozari Takatifu kwa mamia ya vijana mkoani hapa, lengo ni kuwahamasisha vijana hao kumkimbilia Bikira Maria kwa sala katika kipindi hiki cha mwezi wa Rozari, lakini pia kwa maombezi yake aweze kulivusha salama Taifa katika uchaguzi mkuu ujao

Nchimbi alikabidhi rozari hizo muda mfupi baada ya kufungua Kongamano la Vijana katika Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, lililofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha uhasibu, mkoani hapa jana.

“Zawadi pekee ninayoweza kuwapa leo hii ni hizi Rozari Takatifu, huu ni mwezi wa rozari kwa mama yetu na kipenzi chetu Bikira Maria. Naamini tukimkimbilia kwa lolote atatusaidia, tutavuka salama,” alisema Nchimbi.

Kila ifikapo mwezi Oktoba waamini Wakatoliki hualikwa kusali Rozari kwa mwezi mzima, lengo likiwa ni kumuheshimu na kumshukuru Bikira Maria kwa maombezi yake ya kimama kwa wanadamu. Lakini ni fursa pia ya kumwendea na kumshirikisha furaha, shukrani, taabu, changamoto na matarajio.

Aidha, sala ya Rozari Takatifu hutoa nafasi ya kutafakari mafumbo ya maisha ya Yesu Kristu na Maria, katika safari ya wokovu wa mwanadamu.

Kwa wakatoliki na marafiki wa karibu wa Bikira Maria, akiwemo mama Nchimbi, huamini kuwa Rozari ni sala nzuri sana na yenye utajiri wa Neema, ni sala inayogusa kwa karibu Moyo safi wa Mama huyo wa Mungu, lakini pia ni chanzo cha kutamalaki kwa amani katika familia, jamii, taifa na ulimwengu mzima. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com