Mkurugenzi Mkazi wa REPSSI Tanzania, Edwick Mapalala akizungumza wakati wa mafunzo
Timu ya Ulinzi na usalama wa mama na mtoto kutoka Wilaya ya Ukerewe wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kupatiwa mafunzo ya namna ya kutoa msaada wa Kisaikolojia wakati wa majanga.
Mwandishi wetu, Mwanza
Ugonjwa wa Corona (Coovid 19) na majanga mengine kama ajali za moto, vivuko, mafuriko na vimbunga vimesababisha kuundwa kwa timu za kutoa msaada wa kisaikolojia kwa jamii.
Timu hizo zimeundwa katika halmashauri sita za mkoa wa Mwanza baada ya Shirika linalojihusisha na utoaji wa msaada wa kisaikolojia la Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI) kwa ushirikiano baina ya Tamisemi na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) kutoa mafunzo kwa maofisa mbalimbali wa halmashauri hizo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkazi wa REPSSI Tanzania, Edwick Mapalala amesema msaada wa kisaikolojia ni eneo muhimu kwa jamii ili wahanga waweze kuendelea na maisha kama kawaida bila kukata tamaa.
“Kama mnavyojua watoto, wanawake wajawazito, wazee na walemavu ndio makundi ambayo huathiriwa zaidi wakati wa majanga, mafunzo haya ni nguzo,” amesema Mapalala.
Ametaja maofisa waliopatiwa mafunzo hayo kuwa ni Kamati za ulinzi na usalama wa mama na mtoto, wataalamu wa maendeleo ya Jamii, madawati ya Jinsia ya Jeshi la Polisi na walimu.
Alitaja wilaya za Mkoa wa Mwanza ambazo mafunzo hayo yametolewa kuwa ni Magu, Sengerema, Misungwi, Ukerewe, Kwimba na Buchosa.
Awali Mkuu wa Dawati la Jinsia, Wilayani Sengerema Jovita Ezekiel, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa sababu yanaweza kuisaidia jamii kurejea kwenye hali ya kawaida licha ya majanga.
Social Plugin