Taarifa hiyo imetolewa leo Jijini Arusha na Katibu Mkuu Wizara YA Kilimo Gerald Kusaya alipoongea na waandishi wa habari wakati alipotembelea kituo cha TARI Selian kukagua mradi wa Mfumo wa Huduma za Taarifa za Udongo (TanSIS).
“ TARI Selian imefanikiwa kukusanya sampuli za 30,040 za udongo toka kwenye kata za mikoa 18 nchini kwa lengo la kupima na kujua tabia ya udongo ili wakulima na wawekezaji wapate kufahamu aina ya zao kupanda wapi na aina gani ya mbolea kutumia ili kuwa na tija “ alisema Kusaya.
Wizara ya Kilimo inalenga kupata ramani ya kata zote 3,956 nchini ili kurahisisha kazi ya wakulima kutambua apande zao gani mahala gani na kutumia aina gani ya mbegu na mbolea kupitia ushauri wa wataalam wa kilimo alisema Kusaya.
Kusaya aliendelea kusema lengo la serikali ni kusaidia wadau wa sekta ya kilimo waweze kufanya maamuzi sahihi yanayolenga kuongeza ufanisi na tija katika kilimo.
“ Tutaweza kumkomboa mkulima endapo tutakamilisha utafiti wa tabia za udongo nchi nzima na kuwa na ramani inayoonyesha aina za udongo ,mazao gani ya kupanda na aina ya mbolea itakayofaa kwa kila eneo” alisisitiza Katibu Mkuu Kusaya.
Ili kuhakikisha huduma za utafiti wa kilimo zinafika vijijini Katibu Mkuu huyo amesema wizara ya kilimo imeanzisha program maalum ijukanayo kama ‘Mobile Watafiti’ kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.
Programu ya Mobile Watafiti inahusisha watafiti wa kilimo kwenda mikoani na kutoa elimu kwa maafisa ugani juu ya kilimo bora na namna gani watafundisha wakulima kuongeza tija
Kusaya alisema program hiyo kwa kuanzia imehusisha watafiti toka TARI Naliendele kuzunguka mikoa 17 inayolima korosho nchini na kutoa huduma za elimu, teknolojia na ushauri wa kuongeza tija kwenye zao la korosho.
“ TARI Naliendele imeunda timu ya watafiti 11 wanaozunguka katika mikoa yote inayolima korosho ikiwa na wataalam wa ugunduzi wa mbegu bora, agronomia, visumbufu vya mimea, viuatilifu na teknolojia za uzalishaji korosho “ alisisitiza Kusaya
Programu ya Mobile Watafiti inawezesha wataalam kukutana na Maafisa Ugani na wakulima kwenye maeneo yao vijijini na kubadilishana uzoefu na elimu katika kuongeza tija ya uzalishaji mazao,
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Selian Ramadhan Ngatoluwa alitaja faida za kujua tabia ya udongo ni wakulima kutambua matumizi sahihi ya mbolea na viwanda vya mbolea kutengeneza mbolea kulingana na mahitaji ya udongo.
Faida nyingine alisema ni wauzaji na wasambazaji mbolea nchini kuagiza mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na wawekezaji katika kilimo watabaini maeneo ya kuanzisha mashamba kupitia ramani zitakazozalishwa kuonesha tabia za udongo kata zote nchini.
Ngatoluwa aliongeza kusema TARI Selian imeanzisha maktaba (archive) ya kuhifadhi sampuli za udongo za nchi nzima kwa kutumia mfumo wa kimataifa kwa ajili ya matumizi ya utafiti na kumbukumbu.
Mikoa iliyofikiwa na sampuli zake kuchukuliwa na ufanyiwa uchunguzi katika maabara ya TARI Seliani ni Manyara, Kilimanjaro,Arusha,Mwanza,Kagera,Mara,Geita,Simiyu,Shinyanga,Singida,Katavi,Njombe,Songwe,Iringa,Mbeya,Rukwa,Dodoma na Morogoro Mikoa nane (8) iliyobaki kufikiwa ni Ruvuma,Mtwara ,Lindi,Tabora,Kigoma,Pwani na Dar es Salaam na kuwa itakapokamilika itaandaliwa ramani za tabia za udongo kwa kata zote 3,956 za Tanzania bara.
Naye Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt.Godfrey Mkamilo alisema wamefanikwa katika mwaka 2019 kugundua aina 54 za mbegu za korosho nchini na kuongoza Afrika kwa kuwa na mbegu bora .
Dkt. Mkamilo alieleza pia kuwa katika kipindi hicho TARI kupitia vituo vyake iligundua aina 22 mbegu bora za mazao kati ya mbegu aina 40 zilizosajiliwa na wizara ya kilimo nchini na kuwa wanalenga ifikapo mwaka 2025 wafikie kuzalisha tani 5000 za mbegu mbalimbali.
Kuhusu mbegu za korosho Dkt. Mkamilo alisema wataendelea kuhakiksha wakulima kupitia Programu ya Mobile Watafiti wanatambua na kufikiwa na huduma ili uzalishaji korosho ufike tani milioni moja ifikapo mwaka 2025 toka tani 278,000 zinazotarajiwa msimu wa 2020/21.
Katibu Mkuu Kusaya pia alikabidhi trekta jipya kwa TARI Selian aina na New Holland lenye thamani ya Shilingi milioni 70 ili kusaidia watafiti kuzalisha aina nyingi za mbegu ikiwa ni mkakati wa wizara ya kilimo kuvipatia vituo vyote 17 vikuu na vingine 18 nchini kuwa na vitendea kazi vya uhakika.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya yupo mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi kutembelea vituo vya utafiti wa kilimo na kuzungumza na watumishi ili waongeze tija mahala pa kazi na huduma bora kwa wakulima.
Social Plugin