Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa
Shinyanga imefanikiwa kurejesha Shilingi Milioni 27 za Walimu Wastaafu
walioathirika na Mikopo Umiza na mwananchi aliyedhulumiwa na Kamishna Msaidizi
wa Ardhi mkoa wa Mwanza akiwa katika harakati za kutafuta huduma ya kupimiwa shamba lake.
Akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari leo Jumanne Oktoba
20,2020 na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa amesema katika
kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2020,wamerejesha fedha hizo jumla ya shilingi
27,000,000/=.
“Katika fedha hizo kiasi cha shilingi 16,600,000/= ni za walimu wastaafu wawili ambao ni Elias Mihambo na Hamis Chaba walioathirika na mikopo umiza kutoka Kampuni mbalimbali zikiwemo za Malicha Microcredit C.Ltd, Kyanyari CO. Ltd na Mwalimu wa shule ya Sekondari Ibisageni na Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kahumulo wilayani Sengerema”,amesema Mussa.
“Fedha zingine kiasi cha shilingi 10,400,000/= ni za mwananchi aitwaye Gasto Njau
aliyedhulumiwa kwa kuambiwa atoe fedha na Kamishna Msaidizi wa Ardhi kwa mkoa wa
Mwanz kwa ajili ya kupimiwa eneo (shamba) lakini hakupatiwa huduma hiyo ya
kupimiwa eneo lake”,ameeleza.
Amefafanua fedha za Mwalimu Mstaafu Elias Mihambo Katinda
zilichochukuliwa isivyo halali ni shilingi Milioni 45 ambapo tayari kiasi cha
shilingi Milioni 18.5 zilikabidhiwa kwa mstaafu husika awamu ya kwanza Julai
24,2020 na leo amekabidhiwa kiasi cha shilingi 8,100,000/= na fedha zingine
zilizobaki shilingi 18,200,000/= zinaendelea kurejeshwa.
“Fedha za mwalimu mstaafu Hamis Maziku Chaba zilizochukuliwa
isivyostahili ni shilingi 27,500,000/= ambapo tayari kiasi cha shilingi
8,000,000/= zilikabidhiwa kwa mstaafu huyo awamu ya kwanza Julai 24,2020 na leo
tunamkabidhi kiasi cha shilingi 8,500,000/=, fedha zingine zilizobaki kiasi cha
shilingi 11,000,000/= zinaendelea kurejeshwa”,ameongeza Mussa.
Kuhusu mwananchi
Gasto Njau aliyetoa kiasi cha shilingi 10,400,000/= kwa kamishna
msaidizi wa ardhi mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kupimiwa eneo (shamba) lake
lililopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga katika kijiji cha
Pandagichiza lenye ukubwa wa ekari 23 pamoja na kupatiwa hati miliki mwezi
Oktoba 2019 lakini mpaka mwaka huu hajapimiwa wala kupewa hatimiliki ambapo fedha
hizo zimeshalipwa na kamishna huyo.
“Kutokana na muundo wa Idara ya Ardhi hivi sasa mkoa wa
Shinyanga una Kamishna wa Ardhi hivyo TAKUKURU ilimtaka kamishna huyo kurejesha
fedha hizo ili mwananchi huyo aendelee na taratibu za kupimiwa eneo lake kwa kutumia ofisi ya
kamishna wa ardhi wa Shinyanga kama atahitaji kuendelea na zoezi hilo na leo
tumemkabidhi mwananchi huyo fedha zake zote shilingi 10,400,000/=”,ameongeza
Mussa.
Kwa upande wao, Walimu hao wastaafu na mwananchi huyo wameishukuru
TAKUKURU kazi nzuri inayofanya katika kusimamia haki kwa kufanikisha kurejeshewa fedha zao.
Social Plugin