Mratibu wa zao la Korosho kitaifa, Dk. Geradina
Mzena akieleza namna shamba hilo la TARI Naliendele lililopo masigati wilaya ya Manyoni ambalo lina jumla ya ekari 35 litakavyoinua tija ya zao la korosho kwa wakulima wa Kanda ya Kati.
Mzena akieleza namna shamba hilo la TARI Naliendele lililopo masigati wilaya ya Manyoni ambalo lina jumla ya ekari 35 litakavyoinua tija ya zao la korosho kwa wakulima wa Kanda ya Kati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manyoni, Charles Fussi akizungumza.
Baadhi ya Wakulima na Maafisa Ugani kutoka
Halmashauri ya Manyoni wakifuatilia mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho yanayotolewa Kituo cha TARI Naliendele kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho.
Na Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Manyoni
HALMASHAURI ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida imekitengea Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele ekari 35 kwenye kitongoji cha Masigati unapofanyika mradi wa kilimo cha pamoja cha zao la korosho, ili kukiwezesha kufanya tafiti zake ikiwemo kuanzisha programu ya ‘Shamba Darasa,’ lakini pia kulitumia shamba hilo kama kituo cha kuzalisha mbegu bora za korosho kwa mikoa ya Kanda ya Kati.
Akizungumza baada ya kufungua mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima wilayani hapa jana, yanayotolewa na TARI Naliendele kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Charles
Fussi alisema shamba hilo litakuwa chachu ya kupania wigo wa kiuchumi na ni fursa kubwa kwa wana-Manyoni.
“Kituo cha Naliendele na Bodi ya Korosho wamekuwa bega kwa bega na sisi katika kutufuatilia hatua kwa hatua kwenye kilimo cha zao la korosho kwa mafanikio makubwa, na tayari tumewapa shamba kwa shughuli zao za utafiti zaidi wa zao hili, na kupitia hapa Manyoni inatarajiwa kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji mbegu hizo bora kwa mikoa mingine ya Kanda ya Kati,” alisema Fussi.
Alisema mpaka sasa tayari ekari takribani elfu 22 kati ya laki moja zilizotengwa kwa ajili ya kilimo cha korosho zimelimwa na zimepandwa, na kwamba kufikia mwakani wilaya hiyo itaanza kujihakikishia uhakika wa mavuno yake kwa zaidi ya ekari elfu 10
ya zao hilo.
Fussi alibainisha siri ya mafanikio hayo kuwa ni mwamko mkubwa kwa wakazi wa halmashauri hiyo kwa kuitikia wito wa matumizi ya mbegu bora, kufuata maelekezo ya
wataalamu kuhusu kanuni bora za zao hilo lakini zaidi ni kwasababu wakulima wenyewe wameelimishwa na sasa wanafahamu faida ya korosho.
“Ni matarajio yetu baada ya miaka mitano mbele halmashauri yetu itakuwa mbali sana kimapato, lakini hata ustawi wa kiuchumi kwa wakulima waliochangamkia fursa ya kulima zao hili utaongezeka maradufu,” alisema.
Awali Mratibu wa zao hilo kitaifa kutoka Tari Naliendele, Dk Geradina Mzena alisema kutokana na hamasa kubwa ya kilimo cha Korosho kwa mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, na kwa kutambua ongezeko la uhitaji wa huduma za kiteknolojia, kituo hicho tayari kimeanzisha shamba kwa kupanda jumla ya mikorosho 945 ambayo
inatarajia kutoa mbegu bora tani 15 baada ya miaka 3 kuanzia sasa.
“Shamba hili litamsaidia sana mkulima wa kanda hii ya kati, kwanza kupata mbegu kwa urahisi na haraka, lakini litamsaidia kupunguza gharama za kusafiri kufuata mbegu hadi Naliendele Mtwara,” alisema Mzena.
Mratibu huyo alisema azma ya serikali ya Awamu ya Tano kwa sasa ni kuinua tija ya zao la korosho kwa manufaa ya uchumi wa mkulima na upatikanaji wa malighafi bora za viwanda. Kwa muktadha huo TARI Naliendele imejipanga kwa msimu huu kuzalisha tani 150 za mbegu bora za zao hilo ili kukidhi mahitaji kwa wote watakaoanzisha mashamba mapya na wale watakaopanua wigo.
Social Plugin