Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetekeleza mpango wa mafunzo kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa mafuta ya kula kanda ya kati, yaliyofanyika Mkalama, Kiomboi, Sikonge, Urambo, Shelui, Manispaa ya Tabora,Nzega, Igunga, Manispaa ya Singida, Kondoa Irangi, Kongwa, Mpwapwa, Kibaigwa, Chamwino, Itigi, Manyoni, Dodoma jiji na Bahi.
Mafunzo haya yamelenga kuwaelimisha wadau hao juu ya uzalishaji bora, uhifadhi sahihi wa bidhaa za mafuta haswa sehemu za kuuzia, ufungashaji sahihi na salama na umuhimu wa kuzingatia na kuweka taarifa sahihi na muhimu katika vifungashio.
TBS imetoa elimu hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya viwanda, SIDO, maafisa biashara, afya na maendeleo wa wilaya ili kuwajulisha wadau wa mafuta ya kula fursa zilizopo ndani ya Serikali ili kuwawezesha kuboresha bidhaa zao ziweze kukidhi matakwa ya viwango na hatimaye kupananua wigo wa soko la ndani na nje ya nchi na kuwafanya kuongeza uzalishaji utakaopelekea kuinua uchumi wao.
Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora (TBS),Bw. Lazaro Msasalaga aliwashauri wadau hao kuzingatia kanuni za uzalishaji na uhifadhi bora na salama ili kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambayo itawalazimu kuteketeza kwa gharama zao.
Pia aliwashauri kuwasiliana na ofisi ya TBS mara kwa mara pale wanapohitaji msaada wa kitaalamu katika mnyororo mzima wa uzalishaji, uhifadhi na ufungashaji sahihi.
Kwa upande wake Meneja wa Utafiti na Mafunzo (TBS ), Bw. Hamis Sudi Mwanasala alisema mafunzo haya kwa wadau wa sekta ya mafuta ya kula yataendeshwa katika mikoa yote nchini na kwa kuanzia yameendeshwa katika kanda ya kati ikijumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.
"Huu ni mwanzo, kwani Shirika litahakikisha mafunzo kama haya yanamfikia kila mdau na katika ngazi ya chini kabisa, leo tupo kanda ya kati, ila tumeshapita kanda ya kusini, nyanda za juu kusini na kwingineko kwa wadau wa bidhaa nyinginezo"Alisema
Alieleza kwamba mafunzo haoa ni bure na Serikali inagharamia kupitia TBS na tunampango wa kufikia wadau wa mafuta ya kula Nchi nzima" alisema.
Pamoja na mada juu ya bidhaa ya mafuta ya kula TBS inatumia mafunzo haya kuelezea majukumu ya Shirika ikiwa pamoja na yale yaliyokua yakifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa ( TFDA).
Kaimu Mkuu wa Kanda ya kati TBS , Bi Salome Emmanuel aliwasisitiza wajasiriamali ambao bado bidhaa zao za mafuta hazijapatiwa nembo ya bora, kuchangamkia fursa ya bure kwa kutuma maombi ya kutumia alama ya ubora kupitia SIDO ili Serikali iwatambue kama wajasiriamali wadogo na kati na waweze kuhudumiwa bure kwa kuwa bidhaa ya mafuta inaangukia katika kiwango cha lazima hivyo kulazimika kukidhi matakwa ya viwango kwa mujibu wa sheria.
Mafunzo haya yalihusisha wadau walioweza kushiriki katika kumbi mbalimbali zilizoandaliwa lakini vilevile utembelewaji wa moja kwa moja wa wadau hao katika maeneo yao ya uuzaji au uzalishaji kama vile maeneo ya Pandambili (Kongwa),soko kuu la Singida, Tarafa ya Pahi ( Kondoa), soko la majengo (jijini Dodoma), Mitundu ( Itigi), soko kuu la Singida, soko kuu la Nzega, soko kuu la Tabora na kwa wauzaji wa barabarani waliopo wilaya ya Shelui
Lengo ni kuwaelimisha madhara yanayotokea pindi mafuta yanapoanikwa juani kwani mwanga,joto na hewa hupelekea mafuta kuharibika kabla ya muda wa mwisho wa matumizi na kusababisha madhara ya kiafya na kuwaelekeza kuboresha mazingira ya utunzaji kwa kuongeza kivuli cha vibanda vyao na kuweka taarifa za vifungashio.
Mzalishaji wa Mafuta ya kula, Bw. Daud Abel Makala na Muuzaji wa Mafuta hayo Bi.Eunice Maneno ambao walibahatika kushiriki mafunzo hayo katika jiji la Dodoma, walipongeza juhudi zinazofanywa na TBS katika kuhakikisha wanawasaidia wadau wa sekta mbalimbali hususani mafuta ya kula kuzingatia viwango ili kuweza kupata masoko ndani na nje ya nchi na kuwa na ushindani huru sokoni.
Hata hivyo waliitaka TBS kuhakikisha huu mpango wa mafunzo sambamba na kaguzi za mara kwa mara masokoni ni endelevu kwa bidhaa zote na haswa maeneo ya vijijini, ili kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa hafifu na zile zilizokwisha muda wa matumizi au zisizotakiwa kabisa masokoni.
Nao wauza mafuta ya kula katika soko kuu la Singida na Tabora wameiomba Serikali kurahisisha upatikanaji wa vifungashio na kuhakikisha vinauzwa kwa bei nafuu ili hata wajasiriamali wa chini waweze kupaki mafuta yao kwa vifungashio bora na salama tofauti na sasa ambapo wanatumia zaidi vifungashio vilivyokwishatumiwa awali kwa bidhaaa nyinginezo.
TBS ilianza kutoa mafunzo hayo Septemba 21 hadi Oktoba 01, 2020 na kufikia wadau zaidi ya 1700 katika kanda ya kati.
Social Plugin