Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUNDU LISSU ASIMAMISHWA KUFANYA KAMPENI ZA UCHAGUZI WIKI MOJA...MWENYEWE ASEMA ATAENDELEA NA KAMPENI



Mgombea urais kutoka chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA Tundu Lissu amesimamishwa kufanya kampeni kwa muda wa wiki moja (siku saba).

Hatua hiyo imechukuliwa mapema hii leo na Kamati ya Maadili ya Taifa ya Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC).

Katika taarifa yake, kamati hiyo imesema imechukua hatua hiyo baada ya malalamiko yaliyowasilishwa na Chama cha NRA na CCM wakilalamika kitendo cha Tundu Lissu alipokuwa mkoani Mara alipodai kuwa rais John Magufuli ameitisha kikao cha wasimamizi wa Uchaguzi nchi nzima ili kuhujumu Uchaguzi.

Taarifa hiyo pia imesema Lissu alilalamikiwa kutoa kauli za kichochezi pindi alipokuwa akifanya kampeni mkoani Geita.

"Baada ya makubaliano ya kina kamati imekubali kuwa Bw. Tundu Lissu amekiuka maadili ya uchaguzi kwa kutoa lugha chochezi na tuhuma zisizothibitika kinyume cha kanuni," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo,(CHADEMA), Tundu Lissu, amepinga uamuzi wa Tume ya taifa ya Uchaguzi na kusema kuwa ataendelea na mikutano yake ya kampeni siku ya Jumapili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es salaa Lissu ameweka wazi kuwa hatofuata uamuzi wa Tume wakumtaka kutokufanya kampeni kwa siku saba kuanzia tarehe 3/10/2020.

"Kamati kuu ya chama chetu inakutana kesho ili kulijadili suala hili na kulitolea ufafanuzi,msimamo wangu binafsi ni kwamba kampeni zinaendele siku ya Jumapili kama ambavyo imepangawa kwenye ratiba iliyoratibiwa na tume ya taifa ya uchaguzi kwa hiyo msimamo ndiyo huu.Mimi najiandaa kwa mikutano ya kampeni siku ya Jumapili, kamati kuu ndiyo itatokayotoa uamuzi, mimi najianda kwa kampeni kesho kutwa", amesema Lissu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com