Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UCHAFUZI WA MAJI CHANZO MAGONJWA YA MLIPUKO


Na Sitta Tumma, Busega.

Mamlaka ya Serikali Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu, imewaagiza watendaji wa kata na vijiji wilayani hapa, kutumia sheria kuwabana watu wanaochafua mazingira, zikiwamo fukwe za Ziwa Victoria.

Imeelezwa kuwa, uchafuzi unaosababishwa na shughuli za kibinadamu lazima uhitimishwe haraka, ili kuiepusha jamii kupata magonjwa ya mlipuko, ikiwamo homa ya matumbo.

Maagizo hayo yametolewa hii leo na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Konzo Suad, katika shughuli za usafi wa mazingira uliofanyika kwenye fukwe za Ziwa Victoria Nyamikoma.

Usafi huo wa kimazingira ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 21 tangu Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere, alipofariki Dunia akiwa matibabuni Hospitali ya St: Thomas, jijini London, Uingereza, Oktoba 14,mwaka 1999.

"Serikali inataka kuona Uwajibikaji kwa kila mtendaji. Kamati za usafi timizeni wajibu wenu.

"Maji yasichafukiwe," amesema Suad, Afisa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Busega.

Suad aliyekuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo akimwakilisha DC Tano Mwera, amesema magonjwa ya mlipuko ni dhoruba inayohitaji hitimisho la haraka kwa kila mtu kutunza mazingira yanayomzunguka.

Baaadhi ya watu kujisaidia ovyo, kutupa taka, mizoga ya wanyama na kilimo ndani ya mita 60 kando mwa fukwe za ziwa ni uchafuzi wa mazingira, unaotakiwa kuangaziwa kisheria.

Sheria ya Usimmizi wa Rasilimali za za Maji Na 11 ya mwaka 2009, pamoja na mambo mengine, inapiga marufuku uchafuzi wa maji, ambapo kosa lake linatajwa kuwa ni jinai.

Mashirika kadhaa yamehusika katika uratibu wa kazi hiyo, ikiwamo JaneGoodall's, Roots & Shoots Tanzania, YAEE (Busega) na Tanzania Red Cross Society (TRCS).

Mratibu wa shughuli hiyo kutoka Shirika la Roots & Shoots Tanzania, Tumaini Fasso, amesema uchomaji nyavu kwa kutumia mafuta ya taa kandoni na ziwa, inavuruga usalama wa afya.

"Ule moshi na majivu yake yakisombwa na maji hadi ziwani, nalo ni tatizo," amesema Fasso.

Amehimiza jamii kutunza mazingira, vikiwamo vyanzo vya maji ili kuimarisha afya zao dhidi ya magonjwa ya mlipuko, ukiwamo kipindupindu, kuhara damu na homa ya matumbo.

Erimina Mosha, Mtendaji wa Kijiji cha na Nyamikoma, aliyemwakilisha pia mtendaji wa kata hiyo, ametaka kulindwa vyanzo vya maji.

"Mwalo wa Nyamikoma unaingiza takribani watu 1,000 kila siku.

"Naomba kazi hii ya kusafisha fukwe (za Ziwa Victoria) iwe endelevu. Vijiji vingine viige ili kuiepusha jamii yetu kupata magonjwa ya milipuko," Mosha amekaririwa.

Ameutaja ugonjwa wa mlipuko wa homa ya matumbo, unasababishwa na mtu kunywa maji yaliyochafuliwa kuwa ni hatari kwa afya ya jamii.

Baadhi ya wananchi, Seleman Haruna, Musa Daud na Nkwimba Mboje, wakazi wa Simiyu, wameeleza kufurahoshwa na zoezi hilo la fukwe.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com