Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe, Dk. Rehema Nchimbi akizungumza baada ya uzinduzi wa mradi kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Zlatan Milisic |
Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na wawakilishi wa mashrika ya umoja wa mataifa ,wadau wa maendeleo na kmati ya ulinmzi na usalama ya wilaya ya Ikungi
Na John Mapepele, Ikungi
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe, Dk. Rehema Nchimbi leo amezindua miongoni mwa miradi mikubwa iliyowahi kutekelezwa nchini, mradi wa pamoja baina ya Mashirika ya Kimataifa ya UN Women na UNFPA kupitia ufadhiri wa Shirika la KOICA wa “Tuufikie usawa wa jinsia kupitia kuwawezesha wanawake na wasichana”.
Mradi huo utagharimu takribani bilioni 11.5 za kitanzania ambao utatekelezwa katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na Msalala mkoani Shinyanga katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.
Dk. Nchimbi amesema lengo kuu la mradi huo ni kuchangia katika kuwawezesha wanawake na wasichana kuwakwamua kiuchumi na kijamii katika mikoa ya Singida na Shinyanga ili kufikia usawa wa kijinsia ambapo amewataka watendaji wote wa Serikali ambao watatekeleza mradi huo kuwa makini katika utekelezaji wa mradi ili malengo ya mradi huo yaweze kufikiwa.
Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali watendaji ambao kwa namna moja au nyingine hawataendana na kasi ya utekelezaji wa miradi chini ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ambapo amesema mrai huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa KOICA Tanzania, Bi Jieun Mo, walengwa wasio wa moja kwa moja takribani wakazi 40,000 kutoka kwenye wilaya ya Ikungi na Msalala na walengwa wa moja kwa moja 2350 wanawake na wasichana kutoka katika wilaya hizo watanufaika na mradi huu ambapo pia wanaume na wanawake 6000 wa Wilaya ya Ikungi watanufaika kwenye eneo la muingiliano wa hati za ardhi.
Mo ameainisha kuwa shughuli za mradi katika kuwaweza wanawake kwenye eneo la uchumi zitajikiza zaidi kwenye kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana wakulima ili waweze kutumia njia nzuri za kilimo na hali ya hewa katika uzalishaji wa alizeti na kilimo cha bustani, kukuza uuzaji wa pamoja, ujuzi wa ujasiriamali na wakala wa uchumi wa wanawake na kuimarisha usalama wa ardhi na umiliki.
Amesisiza kuwa shughuli hizo zitatekelezeka kupitia kuunda vikundi vya uzalishaji wa kilimo cha bustani kwa wanawake, kuunganisha wanunuzi wa vikundi vya wakulima vya wanawake,kusaidia ujenzi wa ghala kubwa moja la alizeti na kituo cha ukusanyaji kilomo cha bustani ili kuboresha uuzaji wa pamoja na utunzaji baada ya kuvuna,.
Alisema pia watatoa mafunzo ya ujasiriamali na ufikiaji wa habari za kifedha na kufuatilia ushauri wa usimamizi wa biashara na fedha na kukuza umiliki wa ardhi pekee na wa pamoja wa wanawake kupitia utoaji wa Hati za Haki za kimila za Makaazi(CCROs).
Mwakilishi wa UN Women Bi, Hodan Addou ameishukuru Serikali ya Tanzania kuwa ushirikiano wake katika kuhakikisha kuwa mradi huu hatimaye umeanza kutekelezwa ambapo amesema Shirika lake linaunga mkono juhudi za Serikali za kumkomboa mwanamke ili kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia.
Bi Addou amesisitiza kuwa mradi huo utasaidia uwezeshaji kijamii kwa kuwawezesha wanawake kusimamia haki zao, kujenga ujuzi wa ujasiriamali wa wanawake na wasichana kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha mifumo ya kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kupitia kuanzisha na kuandaa vifaa katika madawati matatu ya Polisi ya Jinsia na Watoto.
Aidha alisema pia wataaanzisha vituo vitatu vya huduma ya dharura katika vituo vya wilaya, kuunda nafasi salama ya umma, kujenga uwezo wa nambari ya msaada ya watoto kitaifa, kuunda na kuimarisha Klabu za Wasichana na kuunda Kamati za ulinzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Zlatan Milisic ameipongeza Serikali kwa kuwa na mradi huo na kuongeza kuwa mradi huo unaendana na malengo ya endelevu ya 2030 hususani lengo namba 5 kuhusiana kuwaendeleza wanawake katika nyanja mbalimbali na kuongeza kuwa mwaka 2020 ni mwaka muhimu sana kwa kuwa tunaelekea katika kutimiza miaka 25 ya azimio la wanawake la Beijing.
Ameeleza kuwa malengo endelevu ya 2030 yameeleza kuwa ili kufikia maendeleo ya nchi kumtambua mwanamke ni jitihada muhimu sana katika kuharakisha na kutimiza malengo yote ya maendeleo ambapo ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa karibu sana ili kuhakikisha wanawake wanakuwa chachu ya maendeleo katika nchi ya Tanzania.
Mwakilishi wa UNFPA, Dk. Winfred amesema kuwa uzinduzi wa mradi umelenga kutokomeza aina zote za unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha usawa katika jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha maisha ya wanawake ambapo amesisitiza kitovu cha matatizo ya kijinsia ni wanaume na mila na desturi potofu zinazomtazama mwanamke kwa kumdharirisha hivyo juhudi za makusudi zinatakiwa kufanywa za kuwaweka wanaume mbele ili kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo amesisitiza kuwa kazi nzuri zinazofanywa na Rais John Pombe Magufuli katika Nyanja mbalimbali ndiyo zinazoyafanya jumuiya za kimataifa kuunga mkono kwa kutoa misaada kupitia miradi mbalimbali hapa nchini.
Social Plugin