MAJALIWA : UONGOZI WA NCHI SI JAMBO LA MZAHA WALA MAJARIBIO
Friday, October 09, 2020
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema wananchi wanatakiwa watafakari kwa kina wakati wanapochagua kiongozi kwa kuwa uongozi wa nchi si jambo la mzaha wala la majaribio ni lazima apatikane mtu makini atakayeweza kuwaletea maendeleo.
“Lazima tujue historia yake kiutumishi tusimchague mtu kwa kuwa amepanda kwenye jukwaa kwa mbwembwe, lazima tupate kiongozi atakayeweza kutuunganisha Watanzania wote na atakayetunza amani. Lazima tupate kiongozi atakayewasaidia wanyonge naye ni Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea urais kwa tiketi ya CCM.”
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Oktoba 9, 2020) alipozungumza na wananchi wa jimbo la Mlalo wilayani Lushoto, Tanga katika mkutano ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wote wawachague wagombea wa CCM katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani kwa sababu wanatoka katika taasisi yenye uwezo wa kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali itikadi za aina yoyote. Amesema viongozi hao watakwenda hadi vijijini na kuwatumikia kupitia Ilani.
Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu na kwenda kumchagua Dkt. Magufuli katika nafasi ya urais kwa sababu tayari wameshuhudia kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. “Tukamchague Dkt. Magufuli aendelee kusambaza maendeleo.”
Amesema maendeleo hayana chama hivyo wananchi wote bila ya kujali itikadi za vyama vyao wahamasishane kwenda kumchagua Dkt. Magufuli ambaye ni kiongozi atakayeweza kushirikiana nao vizuri katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao kwa kutumia Ilani ya uchaguzi ya CCM, ambayo imeanisha kila kitu.
Akizungumzia kuhusu usambazaji wa nishati ya umeme Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wananchi hao kwamba vijiji vyote 85 katika wilaya hiyo ambavyo bado havijafikiwa na nishati ya umeme vitafikiwa. Wilaya hiyo ina vijiji 208 kati yake vijiji 123 tayari vimeshaunganishiwa umeme.
Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Lushoto. Gharama za kuunganishiwa umeme huo amezipunguza kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 tu.
Pia Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala hawatalipia fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin