Na. Ivona Tumsime na Peter Haule, WFM, Dodoma
Tanzania imepokea msaada wa Faranga za Uswiss milioni 17.8 sawa na shilingi bilioni 44.1 kwa ajili ya kugharamia Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) na kuchangia Mfuko wa Pamoja wa Afya kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Mkataba wa msaada huo umesainiwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Uswiss nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot kwa niaba ya Serikali ya Uswiss.
Katibu Mkuu, Bw. Doto James, alisema kuwa kiasi cha Sh. bilioni 39.15 ni kwa ajili ya kugharamia Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2023.
“Msaada kwa ajili ya TASAF utasaidia kupunguza umasikini na kuboresha nguvu kazi, kuboresha uwezo wa kununua mahitaji ya kaya masikini, kuongeza uandikishwaji wa watoto shuleni na kuimarisha huduma za jamii”, alieleza Bw. James.
Kwa upande wa msaada wa Mfuko wa Pamoja wa Afya, Bw. Doto James, alisema kuwa utasaidia katika kuboresha utendaji wa watoa huduma ya Afya ya msingi, kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa na kuwezesha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya pamoja na malengo yake.
“Ninaishukuru Serikali ya Uswiss kwa mahusiano mazuri kati yake na Tanzania ambayo yamechangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikuhusisha sekta ya Afya na Sekta za uchumi” alisema Bw. James
Alieleza kuwa Uswiss ni mwanzilishi wa Mfuko wa Afya wa Pamoja ulioanzishwa mwaka 1999 na mchango wake kwa kipindi hicho ni dola za Marekani milioni 36.12, kiasi kilichosaidia kuboresha huduma za afya katika Zaidi ya kaya 184.
Naye Balozi wa Uswiss nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot, alisema kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, theluthi mbili ya misaada ya nchi yake imetolewa kuchangia bajeti ya Mifuko ya Pamoja ya Kisekta na theluthi moja katika mipango ya misaada ya kiufundi pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
“Kusainiwa kwa makubaliano ya msaada wa leo kutaruhusu kuendelea kuchangia Mpango wa Afya kwa wote nchini na tutaendelea kuwekeza katika Mfuko huu”, alieleza Mhe. Balozi Chassot.
Alieleza kuwa wakati Tanzania inapiga hatua kiuchumi na kusababisha ubora wa Maisha kwa watu wengi ni lazima pia kulinda Maisha ya wale ambao hawajanufaika kikamilifu na ukuaji huo wa uchumi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu na Mwenyekiti wa Bodi ya TASAF, Dkt. Moses Kusiluka na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi Joseph Nyamuhanga, wameahidi kuwa Fedha hizo zilizotolewa kama msaada na Serikali ya Uswiss zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuwakwamua wananchi kutoka katika umasikini na kuleta maendeleo stahiki.
Mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF umeingia awamu ya Pili ambapo katika awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 2013 hadi mwaka 2019, kaya milioni 1.1 zenye watu 5,296,470 kwenye Serikali za Mitaa 159 Tanzania Bara na Zanziba, zimenufaika na ufadhili huo.
Hatua hiyo imewezesha watoto milioni 1,805,613 kujiandikisha elimu ya msingi na wanafunzi 448,409 waliosomeshwa elimu ya sekondari katika kaya 1.1 zilizonufaika
Mpango wa Pili wa TASAF ulioanza mwaka 2020/2021, utakuwa wa miaka minne na umepanga kutumia dola za Marekani milioni 883.3 sawa na sh. trilioni 2.02 zitakazo tumika kuzifikia kaya masikini katika vijiji na mitaa ambayo haikufikiwa wakati wa kutekeleza mpango wa TASAF awamu ya kwanza.
Mwisho.
Social Plugin