Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Agri Thamani Foundation,Neema
Lugangira na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa Kituo cha Utafiti wa mbogamboga na matunda cha
Kimataifa cha World Vegetable Center,Dk.Gabriel Rugalema wakiwa kwenye picha ya pamoja huku wakionyesha mkataba
huo baada ya kuusaini.
Na MWANDISHI WETU-ARUSHA
MKURUGENZI wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Agri Thamani Foundation,Neema
Lugangira ,leo (Oktoba 5,2020),amesaini mkataba wa makubaliano kati ya shirika
hilo na Kituo cha Utafiti wa mbogamboga na matunda cha Kimataifa cha World
Vegetable Center,utakaosaidia kuboresha lishe.
Shirika la Agri Thamani lililojikita kwenye kuchangia
kutokomeza udumavu na utapiamlo lenye makao yake makuu mkoani Kagera,linafanya
kazi ya kutoa elimu ya lishe kwenye shule,kaya na jamii na kuhamasisha kilimo
lishe.
Mkataba huo wa makubaliano umesainiwa jijini Arusha
ambapo makubaliano hayo yapo kwenye maeneo saba ikiwemo kuhamasisha ulaji wa
mbogamboga na matunda kama sehemu ya kuimarisha lishe bora na kuwezesha
kutokomeza udumavu na utapiamlo.
Akizungumza wakati wa tukio hilo,Neema ambaye pia ni
Mbunge Mteule wa Viti Maalum(CCM),Kundi la Asasi za Kiraia (NGO’s),Tanzania
Bara,alisema katika mkataba huo wa miaka mitano wanatarajia kuanza kuutekeleza
katika mikoa saba hapa nchini.
Alitaja mikoa hiyo ni Kagera,Tanga,Kigoma,Dodoma, Geita,Tabora
na Kigoma,ambapo wanatarajia kuanzisha bustani za mboga lishe za mfano katika
Shule zote za Msingi na Sekondari za Serikali katika mikoa hiyo ambayo
itaambatana na elimu kuanzia kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Alisema kuwa wanatarajia kuanza zoezi hilo la kuanzisha
bustani hizo mwezi huu katika Manispaa
ya Bukoba,ambapo baada ya kumaliza katika halmashauri hiyo wataanzisha bustani
hizo katika shule zingine za mikoa hiyo saba.
“Tutaanzisha bustani za mboga lishe za mfano kwenye
shule zote,watoto chini ya umri wa miaka mitano,wazee na wenye uhitaji mkubwa
wa lishe.Na tumeamua kuchagua mikoa hii kwa sababu inaongoza kwa changamoto ya
ulaji wa mboga na matunda uko chini,”alisema
Awali Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini
wa kituo hicho,Dk.Gabriel Rugalema,alitaja maeneo mengine waliyoingia
makubaliano ni pamoja na kueneza elimu ya kilimo na lishe kwa jamii,kuweka
msukumo katika ulaji wa mboga na matunda,kusaidia kuanzisha bustani za mboga na
matunda shuleni.
Nyingine ni kusaidia kutunga sera na mipango kazi ya
Taifa rafiki kwa tasnia ya kilimo cha mbogamboga na lishe,kuwafikia na
kuhamasisha waandishi wa habari kama wadau maalum wa kusaidia na kueneza elimu
ya lishe na kuangazia akina mama na vijana katika uzalishaji wa mazao ya
mbogamboga.
Aidha Kituo hicho kilitoa pakiti 500 za mbegu za mbegu
bora za mgoga mchanganyiko zenye viini lishe ambazo ndizo zitaanza kwenda
kutumika kwa ajilli ya bustani hizo za mfano katika mikoa hiyo ambayo inaanza
kutekeleza makubaliano hayo.
“Tutashirikiana kutafuta wadau wengine ambao
tutashirikiana nao ili tuweze kufanikisha hili kwani tumeona ni la muhimu ndiyo
maana tumekubali kushirikiana nao,tunaamini ukipeleka elimu hii kwa wakulima wa
kawaida utajenga uwezo wao wa lishe na kiuchumi kwani Tanzania ina chakula
lakini haina lishe bora,”alisema Dk. huyo