Wakulima Kote Nchi Wataendelea Kupata Mbolea Kwa Bei Nakuu Na Kwa Wakati – Katibu Mkuu Kilimo Gerald Kusaya
Wednesday, October 14, 2020
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya amesema kuwa Serikali imejipanga vizuri ili kuhakikisha Wakulima wote nchini wanapata mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu.
Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo jana, tarehe 13 Oktoba, 2020 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Kimataifa ambapo Kitaifa siku hiyo imeadhimishwa katika kitongoji cha Dakawa, wilayani Mvomelo, mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuhakikisha Wakulima wanapata pembejeo bora kwa wakati na kwa bei nafuu, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Wadau wengine.
“Wizara itaimarisha na kusimamia mifumo iliyopo; Ikiwemo Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea (Bulk Procurement System – BPS) kwa pamoja na tutawashawishi Wadau wa Maendeleo ili waendelee kushirikiana nasi ili kuliletea taifa letu maendeleo kupitia Sekta ya Kilimo”. Amekaririwa Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu Kilimo Bwana Gerald Kusaya ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI) ipo mbio kukamilisha zoezi la kupima sampuli za udongo katika Kata zote nchini ili kufahamu mahitaji ya virutubishi vya udongo wote kuanzia ngazi ya Kata na kwa kufanya hivyo; Wizara itakuwa na kanzi data ambayo itatoa taarifa ya mapungufu ya udongo ambapo ushauri kuhusu matumizi ya mbolea yatafanyika kisasa na kwa usahihi.
Katibu Mkuu amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mbolea ambayo kwa mwaka huu imeadhimishawa katika kitongoji cha Dakawa wilayani Mvomelo mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuzisimamia Taasisi zake zote zilizo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili kuhakikisha Wakulima wanapata pembejeo bora kwa wakati na kwa bei nafuu.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Wizara kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ili kuongeza tija na kuhakikisha mazao ya kilimo yanapata soko lenye bei nzuri kwa kuziimarisha Taasisi ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko CPB) ili zinunue mazao ya kilimo kwa kiwango kikubwa.
Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa Wizara ipo kwenye mapitio ya Sera ya Kilimo ya mwaka 2013 na pamoja na kutunga Sheria ya Kilimo ili kuiwezesha Sekta ya Kilimo kuongeza tija maradufu ili kulifanya taifa kuuza chakula kingi nje ya nchi na kuongeza malighafi za viwandani pamoja na kuongeza mchango mkubwa zaidi ya sasa kwenye pato la taifa.
Siku ya Mbolea Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Oktoba ikiwa ni kumbukizi ya uvumbuzi wa kirutubishi aina ya amonia kinachopatikana hewani, uvumbuzi uliofanywa na Bwana Fritz Haber, Raia wa Ujerumani mwaka 1908.
Siku ya Mbolea Duniani iliadhimishwa kwa mara ya kwanza tarehe 13 Oktoba 2016 nchini Uingereza na hapa nchini Maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya tatu sasa. Kuadhimishwa kwa siku hii ni mpango wa Kimataifa unaoungwa mkono na Jumuiya za Sekta ya Mbolea Duniani kwa lengo la kuelimisha Umma kuhusu matumizi ya mbolea na manufaa yatokayo na matumizi hayo na kutia moyo juhudi za ubunifu katika teknolojia za mbolea katika kilimo kwa mustakabali wa maendeleo endelevu.
Uvumbuzi huo ulichochea mapinduzi ya kijani katika karne ya 20 yaliyowezesha kuongezeka kwa uzalishaji katika kilimo kutokana na matumizi ya mbolea. Mapinduzi hayo yalisaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa janga la njaa na kuleta uhakika wa chakula katika nchi nyingi duniani.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin