Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUTUNZA TAARIFA ZA UTENDAJI WAO WA KAZI KILA SIKU


Na WAMJW – Dar Es Salaam
Wauguzi na wakunga nchini wamekumbushwa kuhakikisha wanatunza vizuri taarifa za kazi kwenye majarada ya kazini kwa kuandika yale yote ambayo wanafanya tangu wanapoingia kazini hadi kutoka.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga katika Hosptali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala – Dar Es Salaam.

“Kila unachofanya kazini aidha umemhudumia mgonjwa au ukiwa na majukumu mengine hakikishen mnatunza taarifa za kazi kwa kuandika kwenye majadara yenu ya kazi” amesema Bi. Ziada

Bi. Ziada amesema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia pia madaktari, wauguzi na wakunga wengine wanaoingia zamu tofauti kutambua kwa haraka nini ambacho kimefanyika na kuweza kuendelea na kazi ambayo wengine wameacha.

Amesema kuwa wauguzi na wakunga wamekuwa wakilaumiwa kwa kutotunza vizuri taarifa za utendaji kazi jambo ambali hupelekea changamtoto kwa wagonjwa kutopata huduma sahihi wakiwa hospitalini.

“Tumekuwa tukilaumiwa hatutunzi kumbukumbu zetu vizuri, andikeni kila mnachofanya, kama umemwita daktari saa 1, hadi saa 3 hajafika andikeni, tufanye ‘documentation’ kadiri inavyowezekana” amesisitiza Bi. Ziada.

Hata hivyo Bi. Ziada Sellah hakusita kuwakumbusha wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa malengo ili waweze kujipima ufanisi wa kazi zao na kujua eneo wanapofanya vizuri na kwenye changamoto.

“Tufanye kazi kwa malengo ili mwisho wa siku tuweze kujipima kwa kufanya tathimini ya malengo tuliyojiwekea kubaini kama tumeweza kuyatimiza” amesema Bi. Ziada.

Amesema kuwa malengo yanaweza kuwa ya siku moja hadi mwaka mmoja kulingana shabaha ulizojiwekea muuguzi au mkunga na yatawaongoza kujua ni wapi walikwama na wapi walifanikiwa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com