Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Waziri Mkuu Atoa Siku Tatu Kwa Wizara Ya Kilimo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa Wizara ya Kilimo kukutana na menejenti ya kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa mbolea ya YARA ili kuhakiki na kupata ithibati ya mbolea ya bure itakayogawiwa kwa wakulima wadogo nchini kupitia mpango wa Action Africa.

Ametoa wito huo leo (Jumatano, Oktoba 7, 2020) alipotembelea kiwanda cha YARA kilichoko jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza kampuni ya YARA kwa uwekezaji mkubwa na utekelezaji wa mpango huo wenye thamani ya shilingi bilioni 16.5.

“Serikali inawashukuru sana YARA kwa kutoa mbolea kwa ajili ya wakulima nchini lakini ni muhimu ithibati ifanyike ili iruhusu mbolea iende kwa wakulima. Mpango huu ni mzuri kwa sababu unaendana na malengo ya Serikali katika kukuza sekta ya kilimo hasa uzalishaji wa chakula”

Waziri Mkuu amesema Serikali ina nia njema ya kuunga mkono wadau wanaosaidia sekta ya kilimo na amewahakikishia wawekezaji hao usalama na mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini. Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa makampuni na taasisi nyingine kuiga mpango huo wa YARA.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amemuomba Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Elizabeth Jacobsen aanzishe Jukwaa la Biashara kwa Wafanyabiashara wa Tanzania na Norway ili wapata uzoefu wa kibiashara kutoka kila upande.

Kwa upande wake, Mkugenzi Mtendaji wa Kampuni ya YARA, Bw. Winston Odhiambo amesema mpango huo utawanufaisha wakulima wadogo 83,000 nchi nzima ambapo tani 12,500 za mbolea ya zitagawiwa bure kwa wakulima wa mahindi na mpunga.

Bw. Odhiambo alisema kuwa mpango huo una lengo la kusaidia uzalishaji wa chakula ambapo wanufaika pia watapewa ushauri wa bure kutoka kwa mabwana shamba wa kampuni ya YARA ili kuleta ufanisi katika uzalishaji.

Naye, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Jacobsen amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya dunia kuhusu uhakika wa upatikanqji wa chakula katika bara la Afrika.

Wanufaika wa mpango huu ni wakulima wadogo kwa ajili ya msimu huu wa kilimo ulioanza Septemba hadi Desemba, 2020 ambao tayari wamekwishasajiliwa kupitia mpango huo.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,       
JUMATANO, OKTOBA 07, 2020.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com