Ujenzi wa Kivuko hicho chenye urefu wa mita 36 na upana mita 12 umefikia asilimia 95 na kinauwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 100. Ujenzi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.3.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa kivuko hicho leo Jumatatu (Oktoba 5, 2020) katika karakana ya kampuni ya Songoro Marine iliyopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Majaliwa amesema ujenzi wa kivuko hicho ni mkakati wa Serikali katika kuendelea kujenga vivuko vinavyokwenda kwenye visiwa vilivyopo nchini.
“Ujumbe kwa wana-Mafia ni kwamba meli hii tunatarajia ianze kuingizwa kwenye maji kuanzia mwezi ujao, baada ya kila kazi kukamilika na TASAC kuja kujiridhisha kwamba ubora chombo hiki umekamilika, tunaamini Wana-Mafia sasa kero yao itakuwa imeisha”
Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi wa Mafia wanasubiri kwa hamu kuona kivuko hicho kikianza safari zake kwa ajili ya kurahisisha huduma za usafiri ikiwamo biashara.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa alitoa wito kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuisaidia kampuni ya Songoro Marine kuhakikisha mzigo wa vifaa vya ukamilishaji wa kivuko hicho unapofika bandarini vinatoka haraka ili Songoro Marine wakamilishe taratibu zao.
Mheshimiwa Majaliwa aliongeza kuwa ujenzi wa vivuko hivyo unawapa uhakika Watanzania wa kuunganishwa na maeneo yote nchini ili kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi, kurahisisha mawasiliano na kurahisisha gharama za usafiri.
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa aliipongeza kampuni ya Songoro Marine kwa ujenzi wa vivuko vyenye ubora wa hali ya juu na kwamba kwa sasa Serikali inauhakika na kampuni ya utengenezaji wa vivuko nchini kwa sababu ya uwezo wake wa kukamilisha kazi kwa wakati na ubora.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 5, 2020.