WIKI YA WATEJA: TIMU IMARA NI CHACHU YA MAHUSIANO MAZURI NA WATEJA NA MAFANIKO YA BIASHARA YAKO

Wiki ya kwanza ya Oktoba ni wiki maalumu ya biashara, kampuni na taasisi kusheherekea umuhimu wa huduma bora kwa wateja na kutambua mchango wa watu wanaohudumia wateja. Kampuni na taasisi mbalimbali zimekuwa zikiitumia wiki hii vyema kudumisha mahusiano na wateja sambamba na kuimarisha timu zinazosimamia mahusiano na wateja. 

Ni wazi kwamba maisha ya taasisi na makampuni yote hutegemea wateja - kuanzia kampuni za utoaji huduma mpaka za uuzaji bidhaa, wateja ni moyo wa kila biashara. 


Mikakati ya biashara nyingi kama siyo zote hujikita katika kuvutia wateja zaidi kwa lengo la kuongeza mauzo. Wataalamu wa masoko wanabainisha kwamba mahusiano mazuri na wateja huitengenezea kampuni au taaisisi mabalozi ambao huchochea ukuaji wa sifa ya kampuni/taasisi husika na kuongeza faida za kibiashara. 

Kuna mikakati mingi ya namna ya kujenga na kusimamia mahusiano kati ya kampuni/taasisi na wateja. Mikakati mingi hujikita katika mawasiliano ya nje ya namna ambavyo kampuni/taasisi inatengeneza chapa yake na kuhakikisha inakuwa na mahusiano mazuri na wateja wake kwa kutoa huduma au bidhaa zinazokidhi viwango sambamba na kuzingatia vigezo vingine kama kuweka bei rafiki na kutoa hisani kwa wateja.

 Kampuni nyingi zimekuwa na vitengo kabisa vya kushughulika na huduma kwa wateja wakati huduma kwa wateja ikifanywa kuwa kipaumbele katika idara zote. 

Ile kauli ya Kiswahili kwamba mteja ni mfalme inaweza kudhihirika kwa kupima namna ambavyo makampuni yanathamini wateja wake. Watoa huduma makini kama watoa huduma za hoteli na ukarimu kwa ujumla wanamjali mteja mmoja mmoja na huhakikisha kwamba pale mteja anapokuwa na malalamiko, hatua stahiki zinachukuliwa kutatua changamoto ili kulinda taswira ya biashara kwa mteja.  

Hivi karibuni, mwanzoni mwa mwaka 2020 mlipuko wa virusi vya corona uliibua changamoto kwa makampuni na taasisi hasa kwa kutikisa mifumo iliyokuwepo ya kusimamia mahusiano na wateja.

 Makampuni na taasisi nyingi hasa zilizojiwekeza katika mauzo ya ana kwa ana, yalikabiliwa na mtihani wa namna ya kuendelea kuonana na wateja na kuendeleza biashara. Corona ilibadilisha utamaduni wa biashara kwa kiasi kikubwa na kufanya mahusiano na wateja kuwa katika mkwamo kwa makampuni/taasisi nyingi. 

Chaguo kubwa lililosalia kwa makampuni mengi lilikuwa ni kuimarisha mifumo ya mawasiliano ya kidigitali na kujengea uwezo waajiri ili waweze kufanya kazi kutoka nyumbani. Chaguo hili linaendana na kaulimbiu ya wiki ya huduma kwa wateja kwa mwaka 2020 ambayo imejikita kuonesha umuhimu wa kuwa na timu imara katika kuboresha mahusiano na wateja. 

Kauli mbiu ya mwaka 2020 ni ‘timu imara’, timu imara ni chachu katika kufanikisha mipango ya ndani ya kampuni yoyote na baadae kusaidia kutafsiri maono ya kampuni au taasisi kwa walengwa ambao ni wateja na wadau wengine. 

Kama ilivyoelezwa katika aya zilizopita, mlipuko wa virusi vya korona umeonesha umuhimu wa kujenga timu imara na namna pia ya kujenga timu imara bila hata kukutana ana kwa ana. Wakati dunia ikipambana kupata tiba ya virusi vya corona, waajiri au/na wamiliki wa makampuni na biashara wamekuwa wakipambana kuendelea kuwa na timu imara itakayofanikisha kampuni kupita katika kipindi hiki kigumu bila kupoteza wateja. 

Waajiri wamekuwa wakiomba ushauri kutoka kwa wataalamu wa rasilimali watu na wasimamiaji wa vipaji ili kuhakikisha wanaendelea kubaki na timu thabiti itakayosaidia kuendeleza biashara zao. 

Kama sehemu ya kusaidia kuimarisha rasilimali watu na kukabiliana na changamoto za biashara wakati na baada ya janga la corona, kampuni inayosimamia masuala ya rasilimali watu, BrighterMonday Tanzania iliandaa na kuzindua muongozo wa kuwawezesha waajiri kusimamia rasilimali watu na kujenga timu imara ili kuimarisha ufanisi na uzalishaji.  

Muongozo wa kusimamia rasilimali watu (Employers Handbook) umeainisha mambo ambayo waajiri wanapaswa kuzingatia ili kuongeza ufanisi katika utendaji. Baadhi ya mambo makubwa katika muongozo huo ni pamoja na; hatua muhimu katika mchakato wa uajiri na ufanyaji maamuzi, mazingira na namna ya kufanya kazi kutokea majumbani au bila kuwepo ofisini na sera za ufanyaji kazi kutokea nyumbani na zana za kuwezesha kufanikisha hilo.

Vilevile, kijitabu cha Mwongozo kwa Mwajiri kimegusia masuala ya mawasiliano yenye ufanisi na wafanyakazi, Usimamizi wa Utendaji na Ustawi wa Wafanyakazi pamoja na mkakati wa rasilimali watu baada ya janga la corona.

Kwa ujumla mwongozo huu unajibia kauli mbiu ya wiki kwa wateja kwani unaonesha jinsi ambavyo mahusiano mazuri na yenye tija baina ya kampuni na wateja yanapaswa kujengwa kuanzia ndani ya kampuni au taasisi. Mwongozo huu unadhihirisha kwamba timu imara ni chachu ya kuimarisha mahusiano na wateja  na timu imara haijitokezi kwa bahati mbaya bali hujengwa kwa kuweka mikakati na mambo yatakayosaidia kuongeza hamasa kwa wafanyakazi/timu ya kampuni husika. 

Kunaweza kuwa na mjadala katika hili, lakini swali rahisi ni kwamba je, kama timu au wafanyakazi hawajahamasika wanaweza vipi kuwashawishi wateja kwamba kampuni wanayoiwakilisha ni nzuri na inatoa huduma nzuri? Mfano mtu anapokwenda benki na kukuta kila anayetoa huduma amenuna na hayuko katika mpangilio mzuri, unafikiri mteja atashawishika kuendekea kuhusiana na benki hiyo?

Utakubaliana na mimi kwamba wiki ya wateja ni wiki ya kujikumbusha umuhimu wa kujenga mahusiano endelevu na wateja wako na hii itawezekana endapo utakuwa na mikakati imara ambayo inaanza ndani na kupevuka kwenda nje. BrighterMonday Tanzania wametupa mwangaza kupitia mwongozo walioandaa kwa mwajiri. Ni muhimu kwa mwajiri na msimamizi wa kampuni au taasisi kujifunza mbinu hizo ili kufikia malengo ya taasisi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post