Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : WORLD VISION YATOA MSAADA WA TAULO ZA KIKE, TV NA VIFAA VYA MICHEZO SHULE 18 SHINYANGA

Mratibu wa Mradi wa ENRICH unaotekelezwa na Shirika la World Vision, Dk. Frank Mtimbwa akimkabidhi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Joachim Otaru moja kati ya maboksi 424 yenye taulo za kike zilizotolewa na Shirika la World Vision kwa ajili ya wanafunzi mkoani Shinyanga.
**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Shirika la World Vision Tanzania limetoa msaada wa Runinga 8,Taulo za kike maboksi 424 na vifaa vya michezo zikiwemo jezi pea 72 na mipira 72 vyenye thamani ya shilingi milioni 62.8 kwa ajili ya shule 18 za msingi na sekondari mkoani Shinyanga. 

Hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo imefanyika leo Jumapili Oktoba 18,2020 katika Chuo Cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi Mjini Shinyanga ambapo Mgeni rasmi alikuwa Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru. 

Makabidhiano hayo ya vifaa yamekwenda sanjari na tukio la kufunga mafunzo ya siku tatu kwa wanafunzi viongozi wa shule za msingi na sekondari 18 zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Kishapu na Kahama Mji ambayo yaliandaliwa na Shirika la World Vision kwa lengo kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu Afya ya Uzazi na Ujinsia na Ukatili wa Kijinsia. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa na kufunga mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru alilishukuru Shirika la World Vision kupitia mradi wake wa ENRICH kwa kutoa mafunzo na vifaa vya michezo na vya kujifunzia shuleni. 

“Nimeambiwa mafunzo mliyopewa pamoja vifaa hivi zikiwemo Tv, Jezi,Mipira na taulo za kike zimegharimu takribani shilingi Milioni 62 na laki 8. Tunawashukuru sana World Vision kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha sekta elimu na kusaidia wanafunzi wetu”,alisema Otaru. 

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaomba walimu na wanafunzi wa shule zilizopata msaada huo wa vifaa vya kujifunzia na michezo kutunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. 

“Nendeni mkatumie Runinga hizi kwa ajili kutoa elimu mbalimbali,lakini pia Walimu hakikisheni taulo za kike zinawafikia walengwa. Takwimu zinaonesha wanafunzi wa kike wanapoteza miezi miwili katika masomo yao wanapokuwa katika siku zao hivyo kupunguza kiwango cha ufaulu. Kutokana na taulo hizi tulizopatiwa ufaulu utaongezeka”,aliongeza Otaru. 

Kwa upande wake,Mratibu wa Mradi wa ENRICH unaotekelezwa na Shirika la World Vision kwa Ufadhili wa Serikali ya Canada katika mkoa wa Shinyanga na Singida, Dk. Frank Mtimbwa alisema shule za msingi na sekondari mkoani Shinyanga zilizonufaika na mafunzo na vifaa hivyo ni zile zilizopo katika eneo la Mradi wa ENRICH katika halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Shinyanga na Kahama Mji. 

Dk. Mtimbwa alizitaja shule hizo kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu kuwa ni shule za msingi Isemelo, Ndoleleji na Kanawa na kwa upande wa sekondari kuwa ni Bulekela,Mangu na Ukenyenge. 

Kwa upande wa halmashauri ya Shinyanga ni shule za msingi alisema ni Manyada,Nshinshinulu na Kituli na shule za sekondari ni Usanda, Tinde na Kituli wakati katika halmashauri ya Kahama Mji ni shule za msingi Penzi, Mwendakulima na Iyenze na shule za sekondari kuwa ni Bugisha, Mwendakulima na Bukamba. 

“Tumetoa taulo za kike maboksi 424,mipira 72 ambapo kila shule itapata mipira minne kwa ajili ya michezo ya mpira wa miguu na pete (miwili kwa wasichana na wavulana miwili),jezi 72 ambapo kila itapata pea 4 (2 kwa wavulana na 2 wasichana) na Runinga 8 kwa ajili ya shule za sekondari zenye umeme”,alieleza Dk. Mtimbwa. 

Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa mama na mzazi mkoa wa Shinyanga, Joyce Kondoro alisema katika mafunzo ya siku tatu kwa wanafunzi 72 kutoka shule 18 mkoani Shinyanga wanafunzi wamefundishwa kuhusu afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana. 

Alizitaja mada zingine ni kuhusu magonjwa ya ngono ikiwemo UKIMWI, ukatili wa kijinsia na namna ya kutoa taarifa kama kuna matukio ya ukatili dhidi ya watoto. 

Nao wanafunzi walioshiriki katika mafunzo hayo akiwemo Nchambi Elias kutoka shule ya Sekondari Mangu wilayani Kishapu walilishukuru Shirika la World Vision kwa kuwapatia mafunzo na vifaa ambavyo vitawasaidia katika kujifunza shuleni.

Afisa Jinsia na Utetezi wa Shirika la World Vision kupitia mradi wa ENRICH, Magreth Mambali alisihi wanafunzi kufanya michezo na kuzingatia masomo yao ili waweze kutimiza ndoto zao.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru akizungumza wakati wa akifunga mafunzo kuhusu afya ya uzazi ya kwa wanafunzi viongozi wa shule za msingi na sekondari 18 zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Kishapu na Kahama Mji ambayo yaliandaliwa na Shirika la World Vision kwa lengo kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu Afya ya Uzazi na ujinsia na ukatili wa kijinsia. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru akiwaomba wanafunzi na walimu kutunza vifaa vilivyotolewa na Shirika la World Vision 
Mratibu wa Mradi wa ENRICH unaotekelezwa na Shirika la World Vision kwa Ufadhili wa Serikali ya Canada katika mkoa wa Shinyanga na Singida, Dk. Frank Mtimbwa akielezea kuhusu mradi wa ENRICH unaotekelezwa katika halmashauri tatu za mkoa wa Shinyanga ambazo ni Kishapu, Kahama Mji na Shinyanga.
Mratibu wa Mradi wa ENRICH unaotekelezwa na Shirika la World Vision kwa Ufadhili wa Serikali ya Canada katika mkoa wa Shinyanga na Singida, Dk. Frank Mtimbwa akiishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na Shirika la World Vision.
Afisa Jinsia na Utetezi wa Shirika la World Vision kupitia mradi wa ENRICH, Magreth Mambali akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa wanafunzi wa shule 18 za msingi na sekondari mkoani Shinyanga na kuwataka wakayatumie vizuri mafunzo hayo na kutunza vifaa vilivyotolewa la Shirika la World Vision.
Afisa Jinsia na Utetezi wa Shirika la World Vision kupitia mradi wa ENRICH, Magreth Mambali akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa wanafunzi wa shule 18 za msingi na sekondari mkoani Shinyanga na kuwataka wakayatumie vizuri mafunzo hayo na kutunza vifaa vilivyotolewa la Shirika la World Vision.
Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa mama na mzazi mkoa wa Shinyanga, Joyce Kondoro akielezea kuhusu mada zilizofundishwa katika mafunzo ya siku tatu kwa wanafunzi 72 kutoka shule 18 mkoani Shinyanga ambapo wanafunzi wamefundishwa kuhusu afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana. 
Afisa Jinsia na Utetezi wa Shirika la World Vision kupitia mradi wa ENRICH, Magreth Mambali (kulia) akimkabidhi Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru ,jezi za michezo kwa ajili ya wanafunzi mkoani Shinyanga.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru (wa tatu kulia) akimkabidhi Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Bakari Kasinyo jezi za michezo kwa ajili ya wanafunzi.
Zoezi la makabidhiano ya mipira ya michezo likiendelea.
Mratibu wa Mradi wa ENRICH unaotekelezwa na Shirika la World Vision kwa Ufadhili wa Serikali ya Canada katika mkoa wa Shinyanga na Singida, Dk. Frank Mtimbwa akimkabidhi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Joachim Otaru moja kati ya TV 8 zilizotolewa na Shirika la World Vision.
Afisa Jinsia na Utetezi wa Shirika la World Vision kupitia mradi wa ENRICH, Magreth Mambali (kulia) akimkabidhi Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru ,TV kwa ajili ya wanafunzi mkoani Shinyanga.
Mratibu wa Mradi wa ENRICH unaotekelezwa na Shirika la World Vision kwa Ufadhili wa Serikali ya Canada katika mkoa wa Shinyanga na Singida, Dk. Frank Mtimbwa akimkabidhi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Joachim Otaru moja kati ya maboksi 424 yenye taulo laini/kike zilizotolewa na Shirika la World Vision kwa ajili ya wanafunzi.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru (wa tatu kulia) akimkabidhi Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Bakari Kasinyo taulo za kike kwa ajili ya wanafunzi.
Mratibu wa Mradi wa ENRICH unaotekelezwa na Shirika la World Vision kwa Ufadhili wa Serikali ya Canada katika mkoa wa Shinyanga na Singida, Dk. Frank Mtimbwa akimkabidhi mipira na jezi Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Bakari Kasinyo (kushoto).
Wanafunzi wa shule za Msingi wakionesha baadhi ya jezi za michezo zilizotolewa na Shirika la World Vision
Wanafunzi wa shule za Sekondari wakionesha baadhi ya jezi za michezo zilizotolewa na Shirika la World Vision.
Nchambi Elias kutoka shule ya Sekondari Mangu wilayani Kishapu akilishukuru Shirika la World Vision kwa kuwapatia mafunzo na vifaa vya michezo, TV na taulo za kike.
Muonekano wa maboksi yenye taulo laini 'pedi' na maboksi yenye TV kwa ajili ya wanafunzi katika shule 18 za halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Kahama Mji na Shinyanga, vifaa ambavyo vimetolewa na Shirika la World Vision.
Muonekano wa mipira na maboksi yenye jezi.
Muonekano wa baadhi ya jezi
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa na mafunzo kuhusu afya ya uzazi ya kwa wanafunzi viongozi wa shule za msingi na sekondari 18 zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Kishapu na Kahama Mji ambayo yaliandaliwa na Shirika la World Vision
Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Bakari Kasinyo akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa na mafunzo kuhusu afya ya uzazi ya kwa wanafunzi viongozi wa shule za msingi na sekondari 18 zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Kishapu na Kahama Mji ambayo yaliandaliwa na Shirika la World Vision.
Wanafunzi wakiwa ukumbini wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Wanafunzi wakiwa ukumbini.
Walimu wakiwa ukumbini

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com