Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DED UKEREWE : KATAENI BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI WATOTO


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ukerewe Bi Esther Chaula
****
Jamii wilayani ukerewe Mkoani Mwanza imetakiwa kuacha tabia ya kuwatoa watoto wao kwenda kufanya kazi za majumbani badala yake wawape elimu ili waweze kutimiza ndoto zao kwani ndiyo msingi wa maisha yao ya baadaye. 

Wito huo umetolewa Novemba 17 na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Bi. Esther Chaula katika hotuba yake ya ufunguzi wa awamu ya pili ya mradi wa kupinga usafirishaji haramu wa watoto na uhamiaji usio salama kwa minajili ya kuwatumikisha kazi hatarishi unaotekelezwa wilayani humo na Shirika la KIWOHEDE kwa ufadhili wa terres des hommes-Netherlands (TDH-NL). 

Alisema kama jamii kila mmoja akitimiza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kuchukizwa na vitendo vya usafirishwaji watoto ukimchukulia huyo mtoto anayefanyia vitendo hivyo kama mtoto wako inawezekana kabisa kumalizia tatizo hilo. 

"Mchukulie yule mzazi ambaye ni rahisi kurubuniwa kirahisi kwamba nipe mtoto ebu jiangalie kwamba yule mzazi ungekuwa ni wewe ndiyo ukawa unarubuniwa wewe ili mtoto wako aende kufanyishwa kazi na kuteseka ungejisikiaje?" alisema.

Aidha aliwataka watendaji wa wilaya na mamlaka za serikali za mitaa kushirikiana na kiwohede katika kutekeleza awamu ya pili ya mradi huo kwani wamekuwa wakifanya shughuli hizi kwa kuinua ustawi wa jamii kwa kufuata misingi ya utekelezaji wa sera na afua zinazowekwa na serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kiwohede Bi Justa Mwaituka aliishukuru ofisi ya Mkurugenzi kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kila mara wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Kwanza niipongeze ofisi yako kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano kwa maafisa wangu kila mara wanapokuja kwako kama unavyofahamu mradi huu una mashirikiano ya karibu na maafisa ustawi, maafisa maendeleo ya jamii, elimu, mipango na idara nyingine kwa kweli Kumekuwa na ushirikiano mkubwa”, alisema.

Aliongeza kuwa katika awamu ya kwanza ya mradi kwa kushirikiana na idara Mbalimbali kama maendeleo ya jamii, dawati la jinsia na watoto pamoja na ustawi wa jamii Wametoa ushauri nasaha, wamefanikiwa kutengeneza mifumo ya upatikanaji wa huduma za afya kwa watoto, wametoa mafunzo mbalimbali ya stadi za maisha, wametoa misaada ya kisheria na kuwarejesha baadhi yao mashuleni kuendelea na masomo. 

Kwa upande wake mratibu wa mradi Amos Juma aliyataja mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya kwanza ni pamoja na watoto 6477 kufikiwa kupitia vipindi vya mafunzo kupitia vilabu mashuleni na mitaani huku watoto 165 wakipewa ushauri wa kisheria na ushauri nasaha pamoja na wazazi 200 kujengewa uwezo wa malezi bora. 

Afisa mradi kutoka Tdh-NL Valence Nkulanga alisema shirika lao linaendelea na shughuli za kuhakikisha hakuna mtoto anayenyonywa huku wakiendelea kutoa ufadhili kwa shirika la kiwohede kuhakikisha wanafanikiwa kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji watoto kupitia mradi huo. 

Mradi huo unafanyika katika vijiji 36 vilivyopo katika Kata 8 ukitekelezwa na Shirika la kiwohede kupitia ufadhili kutoka shirika la kimataifa la terres des hommes - Netherlands(Tdh-Nl). 

Uzinduzi huo wa awamu ya pili ya mradi umefanyika wilayani ukerewe na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wilayani humo akiwemo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri (alikuwa mgeni rasmi) , maafisa maendeleo, maafisa elimu, mkuu wa polisi dawati la jinsia na watoto, viongozi wa dini, viongozi wa serikali ngazi ya kata na vijiji, walimu wa shule, waandishi wa habari na maafisa wa Kiwohede.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwohede Bi Justa Mwaituka akizungumza
Wp Bernadetha afisa wa polisi dawati la jinsia na watoto akitoa mada
Valence Nkulanga afisa mradi kutoka TDH-NL akitoa mada
Washiriki wa uzinduzi wakiwa ukumbini.
Mshiriki akichangia mada
Washiriki wa uzinduzi wakiwa katika picha ya pamoja

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com