Picha haihusiani na habari hapa chini
Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV- Pwani
DIWANI Mteule wa Kata ya Kikongo wilayani Kibaha Vijijini katika Mkoa wa Pwani Fatma Ngozi pamoja na mjukuu wake mwenye umri wa miezi kati ya saba na nane Ajivin Hamis wamefariki baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto usiku wa kuamakia leo Novemba 9,2020.
Tukio la kuungua kwa nyumba hiyo na kusababisha vifo hivyo limetokea saa nane usiku wa kuamkia leo katika eneo hilo ambapo mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Michuzi TV na Michuzi Blog kwamba mbali ya kufariki kwa diwani mteule na mjukuu wake watu wengine watano wameokolewa kutoka kwenye nyumba hiyo.
Wamesema chanzo cha kuungua kwa nyumba hiyo bado hakijafahamika ingawa baadhi ya mashuhuda wanasema huenda ikawa imeungua kutokana na hitilafu ya umeme.Hata hivyo bado haijafahamika kilichosababisha kuungua kwa nyumba hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi kubaini chanzo cha moto huo ambao umesababisha vifo hivyo ili kubaini ukweli ,hivyo bado wanachunguza na watakapokamilisha uchunguzi watatoa taarifa.
Amesema maiti zimehifadhiwa katika Hospitali Mlandizi wakati wakiendelea na uchunguzi na baada ya hapo watakabidhi kwa ndugu kwa ajili ya shughuli za mazishi. Kwa upande wa majeruhi waliokolewa kwenye nyumba hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha.
Hata hivyo ameomba wananchi kutoa ushirikiano na yoyote mwenye taarifa zitakazosaidia kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo ni vema akaziwasilisha katika jeshi hilo wazifanyie kazi.Alipoulizwa chanzo cha moto huo amejibu ni mapema mno, wakikamilisha uchunguzi watafahamu kilichosababisha.
CHANZO - MICHUZI BLOG