Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu, Bi. Gemma Akilimali akielezea umuhimu wa wanaumu kukubaliana na hali halisi ya mabadiliko yanayofikiwa na wanawake kimaendeleo hivyo wawape ushirikiano kwani maendeleo ya kweli yanaletwa na wanaume na wanawake.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala Conchesta Kabete akitoa mada kuhusu Maandalizi ya Bajeti ya Serikali katika ngazi ya halmashauri.
Washiriki wa mafunzo ya jinsia na Bajeti kwa mtazamo wa kijinsia kwa Wanajamii na Watendaji wa vijiji na kata za Shilela na Lunguya halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa UNFPA na KOICA wakipiga picha ya pamoja leo Ijumaa Novemba 13,2020.
Washiriki wa mafunzo ya jinsia na Bajeti kwa mtazamo wa kijinsia kwa Wanajamii na Watendaji wa vijiji na kata ya Lunguya halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga wakipiga picha ya pamoja
Washiriki wa mafunzo ya jinsia na Bajeti kwa mtazamo wa kijinsia kwa Wanajamii na Watendaji wa vijiji na kata ya Shilela halmashauri ya wilaya ya Msalala wakipiga picha ya pamoja.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Wanaume wametakiwa kukubaliana na hali halisi ya mabadiliko yanayofikiwa na wanawake kimaendeleo hivyo wawape ushirikiano kwani maendeleo ya kweli yanaletwa na wanaume na wanawake.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Novemba 13,2020 na Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu, Bi. Gemma Akilimali wakati wa mafunzo ya jinsia na Bajeti kwa mtazamo wa kijinsia kwa Wanajamii na Watendaji wa vijiji na kata za Shilela na Lunguya halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa UNFPA na KOICA.
Gemma amesema wanaume wanatakiwa wakubali kuwa maendeleo katika jamii yanaletwa na wote (wanaume na wanawake) hivyo wajisikie amani kushirikiana na wanawake ambao wanapiga hatua kimaendeleo ikiwemo uwezo wa uchumi ili kuleta maendeleo katika familia ,jamii na taifa kwa ujumla.
“ Wanaume wakubaliane na hali halisi ya mabadiliko yanayofikiwa na wanawake kimaendeleo,mfano uwezo wa kumiliki rasilimali unapopungua kwa wanaume, wasijisikie unyonge na kutumia mfumo dume katika kukabiliana na hali hiyo dhidi ya wanawake. Hivyo wawape ushirikiano kwani maendeleo ya kweli yanaletwa na wanaume na wanawake” ,amesema Gemma.
“Napenda kuwaondoa hofu wanaume kuwa msione wanawake wanataka mabadiliko kwamba wanahitaji kuwapindua bali wanahitaji ushirikiano ili waweze kupiga hatua kimaendeleo hali itakayonufaisha jamii kwa ujumla”,ameongeza Gemma.
Aidha amesema mabadiliko ya mtazamo wa kijinsia yanahitaji mabadiliko ya kijinsia na mabadiliko ya kweli ya kijinsia yanahitaji mabadiliko ya kifikra na kimaono na kwamba njia ya kuleta mabadiliko mazuri ni kusameheana na kutolipiziana visasi.
Katika hatua nyingine amesema ukosefu wa matundu ya vyoo na maji yanaathiri makundi yote ya wanawake waliopo shuleni na ofisini.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo kutoka kata ya Shilela na Lunguya katika halmashauri ya wilaya ya Msalala wamesema vipaumbele vyao ni kupatikana kwa zahanati kila kijiji, barabara,madarasa, vyoo shuleni na maji safi na salama kwani sasa wanalazimika kutumia maji ya visima
Wamesema ili kufikia maendeleo ya kweli ni jukumu la wanawake na wanaume kushirikiana ikiwa ni pamoja na kupendekeza bajeti ngazi ya halmashauri inayogusa maisha ya wananchi wote.
Naye Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala Conchesta Kabete alisema katika bajeti zake serikali inaendelea kuzingatia makundi ya vijana,wanawake na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali.
Soma Pia :