Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndungile akizungumzia magonjwa ya milipuko.
Afisa afya wa mkoa wa Shinyanga Neema Simba akizungungumzia magonjwa ya milipuko
Evarist Kabalo mkazi wa manispaa ya Shinyanga akizungumzia magonjwa ya milipuko na kuwataka wazazi wawe makini kwa watoto wao wasiwaachie wakaokota matunda chini.
Suzy Luhende, Shinyanga
Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndungile amewataka wananchi Shinyanga katika msimu huu wa matunda ya maembe kuosha matunda hayo na kunawa mikono pindi wanapotaka kutumia ili kujiepusha na magonjwa ya milipuko.
Tahadhari hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ambapo amesema nyakati hizi ni msimu wa matunda aina ya maembe ambayo ndiyo yamekuwa mengi, hivyo wananchi wajitahidi kuyaosha vizuri na kunawa mikono kabla ya kuyatumia ili kujikinga na magonjwa ya milipuko.
"Watu wengi katika msimu huu wanatumia matunda mbalimbali lakini mengi ni aina ya maembe ambayo ni msimu wake, kinachotakiwa ni kuyaosha vizuri, kunawa mikono kabla ya kutaka kuyaandaa kuosha chombo cha kuwekea matunda vizuri, na kuhakikisha tunda hilo liko salama halijaoza yaani halijaingiliwa na wadudu wanaoshambulia matunda hayo"amesema Dk. Ndungile.
Kwa upande wake Afisa afya wa mkoa wa Shinyanga Neema Simba amesema ili kujikinga na magonjwa mbalimbali ya milipuko ikiwemo kipindupindu wananchi wanatakiwa wanawe mikono na waoshe matunda wasile ambayo hayajaoshwa na wanaouza matunda hayo wanawe mikono yao vizuri kwa kutumia maji safi na sabuni .
"Pia nawaomba wauza matunda wanaotembeza mitaani watembee na chombo cha kuwekea taka hizo, wanapomenya waziweke ili wasizitupe hovyo wakasababisha nzi kuzagaa na kusababisha magonjwa ya milipuko",amesema Neema.
Nao baadhi ya wananchi wa manispaa ya Shinyanga Evarist Kabalo na Regina Daudi walisema ili kujikinga na magonjwa ya milipuko wauzaji wa matunda wanatakiwa kutembea na maji safi ya kuoshea na kunawa pia wawe na karatasi za kuweza kufuta maji baada ya kunawa mikono.
Kabalo amesema kwa watu wanaoishi vijijini wasipende kuokota matunda yaliyoanguka chini ya mti na kuyatumia bila kuyaosha kwa sababu inawezekana yameangukia kwenye kinyesi cha mtu kwa sababu wengi wanajisaidia chini ya miti wakati wa usiku.
Aidha Regina amesema wazazi wote kuwalinda watoto wadogo katika msimu huu wa maembe wawe makini kwani watoto ni mabingwa wa kuokota maembe na kula pale pale bila kuosha na kusababisha kuugua matumbo mara kwa mara.
Social Plugin