Kamanda wa Polisi, mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao, amesema kuwa moto ulioteketeza nyumba aliyokuwa akiishi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu, Fabian Manoza, ulisababishwa na uwepo wa baadhi ya vifaa mbalimbali vya umeme vilivyokuwa vimechomekwa ikiwemo Friji.
Kamanda Abwao amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana Novemba 14,2020 na wakati nyumba inateketea Mkurugenzi huyo hakuwepo nyumbani, bali aliyekuwepo ni mdogo wake.
"Nyumba yote imeteketea kwa moto, nje kulikuwa na gari nalo kidogo liungue ila lilivutwa, na chanzo cha moto mule ndani, waliacha vitu vikiwa vimechomekwa kwenye umeme, ikiwamo friji, chaji za simu na vingine, nadhani umeme ulicheza ikatokea shida," amesema RPC Abwao.
Aidha Kamanda Abwao ameongeza kuwa wakati wa tukio hilo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika eneo la tukio, lakini wakashindwa kuuzima moto huo, "Mule ndani moshi mzito ulikuwa umetanda sana, hivyo zimamoto hawakuingia na hakuna madhara yoyote kwa binadamu na uchunguzi unaendelea ili kukibaini hasa kiini cha moto huo".
Manoza amesema hakuwepo nyumbani wakati moto unazuka na taarifa hizo amezipokea kutoka kwa mdogo wake aliyekuwepo nyumbani.
"Mimi niko safari. Lakini kwa mujibu wa mdogo wangu aliyekuwepo nyumbani wakati wa tukio, chanzo cha moto hakijajulika," amesema Manoza.
Amesema mdogo wake huyo, alishtushwa usingizini na hewa nzito iliyotokana na moshi uliotanda ndani ndipo alipoanza jitihada za kujiokoa huku akipiga kelele kuomba msaada.
Kwa mujibu wa kwa mujibu wa Manoza moto huo umeteketeza samani na mali zote zilizokuwepo ndani ya nyumba.