Afisa Mkuu wa Programu wa TGNP, Shakila Mayumana akizungumza katika kikao cha wadau wanaofanya kazi na TGNP katika kutetea haki za wanawake na wasichana.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umekutana na wadau inaofanya nao kazi katika kutetea haki za wanawake na wasichana ili kufanya tafakuri ya Mradi wa TAPO: Sauti ya Wanawake na Uongozi-Tanzania unaotekelezwa katika mikoa 9 nchini Tanzania kwa lengo la kukuza usawa wa kijinsia kwa wanawake na wasichana.
Kikao hicho cha Tafakuri ya Mradi wa TAPO: Sauti ya Wanawake na Uongozi kimefanyika leo Jumamosi Novemba 21, 2020 Jijini Mbeya kwa kuwakutanisha pamoja wanufaika wa mradi kutoka Vituo vya Taarifa na Maarifa na wadau wanaotetea haki za wanawake na wasichana, Wafeminia vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika hlashauri ambako mradi unatekelezwa.
Afisa Mkuu wa
Programu wa TGNP, Shakila Mayumana amesema lengo la kikao hicho ni kujifunza na
kushirikishana fursa, uzoefu na changamoto wanazozipata katika kutetea haki za
wanawake na wasichana kupitia Mradi wa TAPO: Sauti ya Wanawake na Uongozi-Tanzania.
“Mradi huu wa TAPO:
Sauti ya Wanawake na Uongozi-Tanzania unaotekelezwa na TGNP kwa ufadhili
wa serikali ya Canada (Global Affairs
Canada) kwa kipindi cha miaka mitano 2019 – 2024 unaotekelezwa na TGNP kwa
ufadhili wa serikali ya Canada (Global
Affairs Canada) lengo likiwa ni kukuza usawa wa kijinsia kwa wanawake na
wasichana”, amesema Mayumana.
“Mradi huu unalenga kuongeza ushirikiano na ujenzi wa nguvu
ya pamoja ili wanawake na wasichana wafurahie maisha na kuongeza usawa wa
kijinsia katika jamii”, ameongeza Mayumana.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Dar es
salaam, Mtwara, Mara, Dodoma, Kilimanjaro, Morogoro, Shinyanga, Kigoma na
Mbeya.
“Kupitia mradi huu
tunataka wanawake na wadau wa haki za wanawake na watoto wafanye kazi kwa
pamoja ‘wajenge TAPO kwa pamoja’ ili
kuwa na sauti ya pamoja kuhusu masuala ya wanawake na wasichana itakayowezesha
kuwa na sheria na sera rafiki kwa wanawake na wasichana”, amesema Mayumana.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Shirika la
AGAPE ACP linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto, John Myola
amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto ili iwe rahisi kujua
changamoto zao na kuepuka kuwaita majina yasiyofaa.
Pia Myola amewakumbusha wazazi kuwa makini na watu wanaokaa
na watoto kwani baadhi yao siyo wema wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya ukatili
watoto ikiwemo kuwabaka na kuwapa ujauzito.
“Watoto wetu wanafanyiwa ukatili na kubakwa na watu wa
karibu kabisa wakiwemo wajomba,
mashemeji, kaka na baba wadogo na wakubwa. ukiwa karibu na mtoto wako
atakueleza matendo anayofanyiwa lakini kama haupo karibu naye, unatumia lugha
mbaya kamwe mtoto huyo hatakueleza yanayomsibu”, ameongeza Myola.
Naye Beatrice Yohana Kimambo kutoka Kilimanjaro amewataka
wazazi na walezi kutoa ushirikiano katika kesi za matukio ya ukatili dhidi ya
watoto badala ya kuendekeza rushwa ili kuzima kesi hizo.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga, Joseph Swalala ameishukuru TGNP kwa kutoa mafunzo kwenye
vituo vya taarifa na maarifa ambapo sasa vituo vya taarifa na maarifa vimekuwa
mstari wa mbele kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia mara tu
yanapotokea.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa Mkuu wa Programu wa TGNP, Shakila Mayumana akizungumza katika kikao cha wadau wanaofanya kazi na TGNP katika kutetea haki za wanawake na wasichana ili kufanya tafakuri ya mradi wa TAPO: Sauti ya Wanawake na Uongozi-Tanzania unaotekelezwa katika mikoa 9 nchini Tanzania kwa lengo la kukuza usawa wa kijinsia kwa wanawake na wasichana leo Jijini Mbeya. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Afisa Mkuu wa Programu wa TGNP, Shakila Mayumana akizungumza katika kikao cha wadau wanaofanya kazi na TGNP katika kutetea haki za wanawake na wasichana.