Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TARURA YADHAMIRIA KUUNGANISHA WILAYA YA RUANGWA NA LIWALE

Ujenzi wa Daraja la Mto Mbwemkuru lenye urefu wa Mita 75 lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi linalojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ukiwa unaendelea. Daraja hili ni mpango wa kuunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale kwa lengo la kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
**


Na Bebi Kapenya - Lindi

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umeendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi ikiwemo ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru lenye urefu wa mita 75 linalojengwa katika barabara ya Chikwale hadi Liwale kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.5.

Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka Nalupi alisema mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru umetokana na mpango wa kuunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale kwa lengo la kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo na kuwezesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa haraka.

“Wilaya hizi mbili ni maarufu sana katika kilimo cha korosho na ufuta, lakini pia wananchi wa vijiji vya Nangurugai, Mirui, Narungombe, Machang’anja na Chikwale watapata faida ya kiuchumi kwasababu mazao yao ya biashara yataweza kuvushwa kutoka upande wa Liwale kwenda Ruangwa ambapo kuna soko kubwa la mazao ya biashara pale Ruangwa mjini”, alisema Meneja huyo.

Mhandisi Nalupi alieleza kuwa hadi sasa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imeshapokea fedha Shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru na ujenzi utakuwa wa Awamu II ambapo Awamu ya I itakuwa ujenzi wa daraja lenyewe kwa kutumia Mkandarasi anaitwa Nyumbani Construction Company Limited kwa mkataba wa Bilioni 1.6 na Awamu ya II itakuwa ni ujenzi wa Makalavati makubwa upande wa Liwale kwa Mkandarasi anaitwa Lumo Cones ambaye ameshaingia mkataba na ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni.

Naye, Bw. Abdallah Nampundai Mkazi wa Ruangwa ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo kwani utanufaisha wananchi kusafirisha mazao yao na kufanya biashara zao.

“Kwa sisi wafanyabiashara na wakulima tunatoa mazao yetu kutoka Ruangwa kupeleka Liwale na tunatoa Liwale kupeleka Kilwa hivyo kukamilika kwa daraja hili kutatusaidia sana kupitisha mazao yetu kwa urahisi”, alisema Bw. Nampundai.

Kwa upande wake, Bw. Leonard Abel Mkazi wa Kijiji cha Nangurugai ameishukuru TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo kwani litakapokamilika litarahisisha usafiri kwasababu wanapata changamoto nyingi mvua ikinyesha ikiwemo kupoteza ndugu zao kwavile Mto huo una mamba wengi hasa kipindi cha mvua hivyo kukamilika kwake kutawasadia sana kwenye suala la usafiri.



Mbali na ujenzi daraja la mto Mbwemkuru, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imekamilisha ujenzi wa Barabara za Lami Ruangwa mjini jumla ya Kilomita 8.32 kwa fedha za Mfuko wa Barabara pamoja na fedha za mradi wa Mfuko wa Umoja wa Ulaya, pia wameweka taa za barabarani jumla ya Km 7.62 mradi uliofadhiliwa na REA (Wakala wa Umeme Vijijini).

Aidha, Meneja huyo alisema kuwa wameweza kuunganisha sehemu kubwa ya Mji wa Ruangwa kwa barabara za Lami ambapo imeweza kurahisisha mawasiliano kwa watumiaji wa barabara na kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo kwavile biashara zimeendelea kufanyika hadi nyakati za usiku kwasababu ya uwepo wat aa za barabarani.

TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa inaendelea na kazi mbalimbali za kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja ili kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa urahisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com