Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Vijana wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kama fursa ya kutangaza kazi zao na kutetea haki za wanawake na watoto badala ya kutumia kwa mambo yasiyofaa katika jamii kama vile kusambaza zisizo na maadili.
Rai hiyo
imetolewa Novemba 20,2020 na Katibu wa Jukwaa la Vijana Wafeminia kutoka
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Zawadi Kondo kwenye Warsha ya Mtoto wa kike,
Teknolojia na Ubunifu wakati wa Tamasha la 6 la Jinsia wilaya ya Mbeya katika
uwanja wa kijiji cha Hatuelo kata ya Ijombe halmashauri ya Mbeya.
Kondo
alisema Mitandao ya Kijamii ikitumika vizuri ni chachu ya maendeleo hivyo
kuwataka vijana hususani wa kike kuacha kusambaza vitu vya hovyo mitandaoni na
badala yake watumie kama fursa ya kutangaza kazi wanazofanya na kuelimisha
jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
“Ukitumia
vizuri mitandao ya kijamii utapata faida. Naomba mtumie kwa ajili ya kujiletea
maendeleo”,alisema.
Kondo
alieleza kuwa Mitandao ya Kijamii imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa watetezi
wa haki za wanawake na watoto kufuatilia matukio ya ukatili yalipo pindi
yanaporipotiwa na kwamba inasaidia kufanya uchechemuzi.
Kwa upande, Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana
Wafeminia Alphonsina Ambrose aliwataka wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wao
kufanya vitu wanavyopenda kufanya na kuwapeleka shule watoto wenye ubunifu ili
kukuza ubunifu wao.
“Mzazi mpe
nafasi mtoto afanye vitu anachokipenda akifanye kwa usahihi ilmradi viwe vitu
vizuri. Mzazi asikilize maoni ya mtoto wake lakini katika kufanya hayo mzazi
asiache kumpa haki ya elimu ili kuboresha ubunifu wa mtoto”,aliongeza
Alphonsina.
“Hata kama
mtoto ana ubunifu mkubwa kiasi gani ni lazima apelekwe shule. Elimu anayopata
itamsaidia kuboresha kazi zake za ubunifu ili kumtengenezea maisha mazuri na
hatimaye kujenga jamii yenye usawa”,aliongeza.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi aliwasisitiza vijana na wanawake kuwa
wabunifu katika kazi wanazofanya na kutumia fursa walizonazo kujiletea
maendeleo ikiwa ni pamoja kuhakikisha wanaongeza thamani kwenye mazao
wanayolima.