Aidha, IGP Sirro ametoa wito kwa viongozi wa siasa wanaosema wanatishiwa usalama wao kuripoti kwenye vyombo vya usalama na sio kukimbilia nje ya nchi.
"Uchaguzi ulikwenda vizuri na nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wadau wote wa uchaguzi, viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa sana. Kuna watu walijipanga kufanya vurugu mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 kukamilika kwa maeneo yote ya Tanzania bara na visiwani, lakini jeshi la polisi tulibaini mapema na kudhibiti njama hizo.
“Jeshi la Polisi lilikamata watu na mabomu kadhaa visiwani Zanzibar, ambao walilenga kulipua ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), vituo vya mafuta pamoja na majengo makubwa ya serikali. Hali ya nchi yetu ni shwari sana hatuna matukio makubwa ya uvunjifu wa amani.
“Hakukuwa na maandamano ya amani yaliyopangwa, bali mtego wa kuliingiza taifa katika fujo, kuna baadhi ya viongozi wa Chadema, Tundu Lissu na wengine kama Godbless Lema walidai kutishiwa kuuawa jambo ambalo siyo kweli. Tanzania tuko salama, niwaambie tena Lissu na Lema na wengine waliokimbia nchi warudi, Tanzania iko salama waje tujenge nchi.
“Wakati ndugu yetu Tundu Lissu alipokwenda ubalozini akisema anatishiwa, niliandika barua aje basi atuambie anatishiwa na nani, lakini habari ya kutishiwa wewe unaweza ukagombana na mtu akakutishia, kama umetishiwa unatoa taarifa polisi. Jeshi la polisi lilimuita mara kwa mara Tundu Lissu aje atoe ushirikiano juu ya tukio lake la kupigwa risasi kule Dodoma, lakini hakutaka kufanya hivyo ,” amesema Sirro.
Kuhusu hali ya amani mkoani Mtwara, IGP Sirro amesema vyombo vya ulinzi na usalama vipo kazini na amewatahadharisha wale wote wanaotaka kujaribu kujiunga na makundi yanayotishia amani ya nchi kuwa sheria zitachukuliwa.