Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi amesema
amejipanga kikamilifu kuhakikisha anatekeleza ahadi zote alizozitoa wakati wa
Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020 huku akisema hatowavumilia wale wote wenye nia ya
kutaka kumkwamisha katika malengo yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Katambi ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 30,2020 wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga
kwenye kikao kilichohudhuria pia na Mstahiki Meya Mteule wa Manispaa ya
Shinyanga, Mhe. David Nkulila,Madiwani na viongozi wa CCM.
Katambi amesema kipindi cha uchaguzi kimeisha hivyo kinachotakiwa
sasa ni kuchapa kazi ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi kuwaondolea
maumivu waliyonayo.
“Mimi Mbunge kwa kushirikiana na madiwani,viongozi wa chama na
serikali pamoja na wananchi hatutakuwa tayari kucheka na mtu ambaye
hatatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM. Kwa kweli hatutakuwa na simile na
atakayetukwamisha”,amesema Katambi.
“Shinyanga tunahitaji maendeleo,tunataka kuubadilisha mkoa huu
lakini pia kuifanya Manispaa ya Shinyanga kuwa Jiji. Haiwezekani mkoa huu mama
unazidiwe maendeleo na mkoa wa Simiyu,lazima sasa tuupe heshima mkoa huu. Pia
kula fedha ya serikali ni marufuku”,ameeleza Katambi.
Katambi amesema sasa ni wakati wa kutekeleza ahadi alizoahidi
ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta ya kilimo,kujenga soko la kisasa, stendi ya
kisasa,kiwanda cha nyama na ajira.
Katika hatua nyingine amesema kuanzia wiki ya pili ya Mwezi
Desemba ataanza kufanya ziara kwenye kata kwa ajili ya kuwaeleza wananchi
kuhusu mipango mikakati aliyoweka katika kutekeleza ilani ya CCM.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya Mteule wa Halmashauri ya Manispaa
ya Shinyanga, Mhe. David Nkulila amesema amejipanga kusimamia nidhamu ya fedha
katika halmashauri hiyo na kwamba hatakubali kuona malalamiko juu ya miradi yanaendelea
kuwepo.
“Maendeleo yote yanahitaji fedha,ni lazima tuwe na nidhamu ya
fedha. Nitafanya kazi usiku na mchana nikishirikiana na madiwani, mbunge,
viongozi wa chama na serikali pamoja wananchi ili kuhakikisha tunaleta
maendeleo katika jamii”,amesema
Nkulila.
“Mkuu yeyote wa Idara katika halmashauri atakayethubutu
kutukwamisha itabidi atupishe. Sitakubali malalamiko yaliyokuwepo yaendelee
kuwepo na hatutasubiri hadi kiongozi wa kitaifa kuja kututatulia kero zetu”,ameongeza Nkulila.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakari Gulam
Mukadam amesema Chama Cha Mapinduzi kimejiandaa kutekeleza Ilani ya CCM kwa
kasi kubwa kwa asilimia 100 na kwamba madiwani na mbunge watapanga siku maalumu
kwa ajili ya kusikiliza kero na matatizo ya wananchi.
Social Plugin