LUKUVI APOKEA TAARIFA YA AWALI YA UHAKIKI ENEO LA MGOGORO MTAKUJA DODOMA
Wednesday, November 04, 2020
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepokea taarifa ya awali ya uhakiki wa eneo lenye Mgogoro la Mtakuja lilipo Kata ya Chang’ombe mkoani Dodoma.
Taarifa ya uhakiki wa eneo hilo lenye ukubwa hekta kumi uliwasilishwa leo tarehe 4 Oktoba 2020 katika ofisi za Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Uratibu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Luge kwa niaba ya timu inayofanya uhakiki kwa wakazi wanaoishi eneo hilo.
Uwasilishaji taarifa hiyo unafuatia kukwama kwa mara kadhaa mazoezi yaliyofanyika huko nyuma na kusababisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuelekeza kufanyika uhakiki mwingine ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa muda mrefu kwenye eneo hilo.
Kwa mujibu wa Kmaishna Msaidizi wa Ardhi Uratibu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Luge, tayari timu ya uhakiki mgogoro huo imeshawapitia wananchi 750 kati ya 1,025 watakaofanyiwa uhakiki.
Luge alisema, kazi kubwa inayofanywa na timu ya uhakiki ni kupitia taarifa ya kila mwananchi na kuangalia hali ya maendelezo yaliyofanyika katika kila eneo la mwananchi analomiliki.
Mazoezi ya uhakiki eneo la Mtakuja Kata ya Chang’ombe mkoa wa Dodoma yamefanyika mara kadhaa katika miaka ya 2005, 2008 na 2015 ambapo zoezi linaloendelea sasa linatarajiwa kuleta suluhu ya mgogoro huo.
Uwasilishwaji taarifa ya uhakiki wa mgogoro wa eneo la Mtakuja Dodoma, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, Naibu wake Nocolaus Mkapa, Kamishna wa Ardhi Nathaniel Nhonge na Watendaji wa Wizara, Jiji la Dodoma pamoja na wa Kata ya Chang’ombe.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin