MARAIS WA AFRIKA WAMPONGEZA JPM KWA USHINDI WA KISHINDO
Friday, November 06, 2020
Na Anitha Jonas – MAELEZO
Marais waliyohudhuria sherehe za kuapishwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli wampongeza kwa ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliyofanyika hivi karibuni pamoja na kuwapongeza watanzania kwa kumaliza zoezi hilo kwa amani.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni alisisitiza kuwa ushiriki wa nchi mbalimbali za Afrika katika sherehe hiyo ni matunda ya msimamo thabiti wa Hayati Baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere na baadhi ya viongozi wa Afrika ambao hawakukubali kuwa vibaraka wa mataifa ya nje.
“Napenda kutoa pongezi kwa watanzania kwa kufanya uchaguzi salama na kumaliza bila vurugu zozote pia na toa pongezi kwa Rais Magufuli kwa ushindi wa kishindo kwani ameshinda kwa kura nyingi pamoja na wabunge mbalimbali wa chama cha CCM nao nimewaona wameshinda kwa kura nyingi, nilikuwa nikifuatilia matangazo ya matokeo ya uchaguzi kupitia televisheni ya TBC 1,” alisema Museveni.
Pamoja na hayo naye Rais wa Comoro, Azali Assoumani alitoa pongezi kwa Rais Magufuli huku akisisitiza kumuombea katika majukumu yake aliyopewa ya kuwatumikia na kuwaongoza Watanzania ili aweze kukamilisha kazi hiyo kama ilivyo desturi ya viongozi kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi kwa msaada wa Mungu.
Naye Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emmaerson Mnangagwa alitoa pongezi kwa watanzania na kutoa salamu kutoka wananchi wa Zimbambwe ambapo alisisitiza kuwa Zimbabwe wanaiangalia Tanzania kama baba na mama wa uhuru wa taifa lao kama alivyowasisi Hayati Mwl. Julius Nyerere.
“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu katika kipindi alichokuwa Mwenyekiti wa SADC alikuwa kinara wa kusimamia kuondolewa kwa vikwazo mbalimbali ambavyo Zimbabwe tulikuwa tumewekewa kwa kutangaza tarehe 25 Oktoba,2020 kuwa siku maalum ya kupinga vikwazo hivyo ikiwa ni maamuzi ya Jumuiya ya SADC,” alisema Rais Mnanangwa.
Halikadhalika nae Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Botswana , Slumber Tsogwane alitoa salamu kwa niaba ya Rais wake Mokgweetsi Masisi kwa kumpongeza Rais Magufuli kwa ushindi wa kishindo huku akieleza sababu mbalimbali zilizomfanya rais wake ashindwe kushiriki sherehe hiyo kwa kubanwa na majukumu ya kitaifa, pamoja na hali ya kuhitajika kukaa karantini mara baada ya kurejea nchini kwa siku kumi na nne atakapotoka nje ya nchi kutokana na hali ya ugongwa wa Corona .
Aidha, Katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliwashukuru watanzania kwa kujitokeza kumpigia kura kwa wingi na kumpa ushindi wa kishindo na alisisitiza kuwa uchaguzi kwa sasa umekwisha na hivyo ni wakati wa kuchapa kazi na kulijenga taifa.
“Napenda kuwapongeza viongozi wote wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia zoezi la uchaguzi vyema na kuhakikisha linaendeshwa kwa uwazi na haki, pia nawashukuru watanzania wote kwa kuwa wazalendo na kulinda amani ya taifa na mara baada ya uchaguzi,” alisema Rais Magufuli.
Akiendelea kuzungumza mara baada ya uapisho huo, Rais Magufuli aliahidi kuendelea kusimamia miradi mikubwa yote aliyoianzisha na kutekeleza mingine mipya pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za taifa na kukuza uchumi, ikiwemo kutatua changamoto ya ajira kwa vijana pamoja na mapambano dhidi ya rushwa.
Sherehe hizo za uapisho zilihudhuriwa na Marais watatu, Mabalozi takribani themanini, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar na viongozi mbalimbali kutoka nchi za Afrika wakiwemo mawaziri wa nchi mbalimbali na viongozi wa mashirika ya kimataifa.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin