Na Godwin Myovela, Singida
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Singida aliyemaliza muda wake, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mtamaa mkoani hapa, Gwae Chima Mbua, amesema mpaka sasa anajivunia kuiacha manispaa hiyo ikiwa inashikilia cheti cha hati safi kutokana na usimamizi madhubuti uliojengwa katika misingi ya nidhamu, hususan kwenye eneo la makusanyo na matumizi ya fedha za umma.
Akizungumza na vyombo vya habari mkoani hapa leo, vilivyomtaka aeleze kwanini anastahili tena kupewa dhamana ya nafasi ya umeya na si diwani mwingine, alijibu kila mgombea hupimwa kwa uwajibikaji wake na sio kimitazamo wala mihemko.
Alisema mpaka alipokabidhi ofisi hiyo hivi karibuni, aliacha manispaa hiyo ikiwa kwenye makusanyo ya takribani asilimia 83, sambamba na kufanikiwa kuwaunganisha madiwani na watumishi katika kuendelea kuijenga Singida kwa kasi na muktadha unaoendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.
“Nawashukuru madiwani na serikali walinipa ushirikiano mkubwa sana, lakini nidhamu, uadilifu na kasi tuliyokwenda nayo vilichochea kasi ya maendeleo yetu hadi kuzivutia hata halmashauri nyingine zipatazo 19 kutoka maeneo tofauti nchini kuja kujifunza- hasa kupitia umahiri wa mradi wa stendi ya misuna,” alisema Mbua.
Alisema mpango uliopo kama atapata ridhaa ya kuchaguliwa tena, ni kuchagiza kwa kuharakisha mchakato wa maboresho ya soko la vitunguu kwa kuhakikisha linawekewa miundombinu ya kisasa ikiwemo zege na lami kwenye barabara zinazolizunguka ili kuondoa kero ya tope na mazingira yasiyo rafiki hasa wakati wa mvua.
Alisema tayari manispaa hiyo imefanikiwa kufungua akaunti maalumu ya mikopo ya akina-mama, hivyo jukumu lililo mbele yake kama atapata ridhaa ni kuimarisha fursa hiyo kwa ustawi wa maisha ya wanawake wa singida, lakini shabaha kubwa ni kuhakikisha makusanyo yanapanda kwa zaidi ya asilimia 83.
Mbua alisisitiza kama atachaguliwa tena ataendelea kuhamasisha nidhamu ya matumizi ya fedha kama alivyofanikiwa kwa miradi mbalimbali iliyotangulia, ikiwemo ule wa fedha zilizotolewa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
“Tunakwenda vizuri na kwa kasi ya aina yake, natamani kuiona singida ikiwa jiji…kwa sasa kuna maeneo fulani tayari yameshaanza kuitwa Ubungo, naitamani singida isiyo na rushwa, singida ya maendeleo ya kweli,” alisema Diwani huyo wa Mtamaa na kuongeza:
“Bado kuna mambo mengi ya kuweka sawa mathalani pale stendi bado tunahitaji kufunga CCTV Camera, lakini tunahitaji kukamilisha mchakato wa kutenga maeneo ya viwanda, kupima viwanja zaidi, kujenga machinjio ya kisasa, kuboresha mifumo ya ukusanyaji taka, pamoja na kuboresha soko letu la vitunguu.”
Mipango mingine iliyopo kama atapata ridhaa ni kuhakikisha anasukuma kwa kasi ujenzi wa soko la kisasa litakalojengwa eneo la Mandewa nje kidogo ya manispaa hiyo, sambamba na kuboresha ‘High Schools’ za Mungu Maji na Mandewa, juhudi ambazo anashukuru kwamba zinaungwa mkono na serikali.
“Nina nia njema ya kuwatendea haki watu wa manispaa ya Singida kwa nafasi ya Meya, suala kubwa ni kuleta maendeleo na faraja,..lakini pia kuunga mkono kwa vitendo kasi ya mheshimiwa Rais katika kuifanya manispaa yetu kuendelea kuwa njema tena njema sana,” alisema Gwae Mbua.