Na Beatrice Sanga, MAELEZO
MBUNGE wa jimbo la Kongwa ambaye alikuwa mgombea pekee wa nafasi ya Spika katika Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amechuguliwa kuwa Spika wa Bunge hilo kupitia kura zilizopigwa na wabunge waliohudhuria kikao cha kwanza cha bunge hilo baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika leo Oktoba 28,2020 kilichofanyika katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.
Ndugai amepigiwa kura na wabunge 345 na kupata asilimia 99.7 za kura zote zilizopigwa ambazo zimemuwezesha kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili.
Akizungumza mara baada kuchaguliwa, Ndugai amewapongeza wabunge wote walioaminiwa na kupewa nafasi na wananchi ili waweze kuwasemea changamoto zao na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuwaletea maendeleo Watanzania waliowapa nafasi kwa kuwa wamewaamini na ndiyo maana wakawatuma ili waweze kuletewa maendeleo kupitia wao pamoja na kushikriki vyema katika utungaji wa sheria.
“Ni heshima kubwa sana, matarajio ya wananchi wenu ni makubwa sana kwa kila mmoja wetu, tunao wajibu mkubwa mbele yetu wa kuhakikisha kwamba hatuangushi matumaini ya wananchi. Watanzania hawa waliotuamini tuwe wawakilishi wao katika nyumba hii tukufu na nina amini kila mmoja hatasahau hata mara moja jukumu la msingi la uwakilishi na kutunga sheria zilizo bora.” Amesema Ndugai
Aidha, ameongeza kuwa kazi za Bunge lazima zionekane na wananchi wanatakiwa kupewa taarifa ya nini kinachoendelea bungeni na ameviomba vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kutoa kazi za bunge ili ziweze kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi ili waweze kujua mambo ambayo viongozi wao wanawasemea Bungeni
Spika Ndugai amesema kuwa yuko tayali kuliongoza Bunge hilo kwa haki na usawa bila ubaguzi na atakuwa mstari wa mbele kutatua matatizo ya wabunge na kuhakikisha anashughulikia kwa ukaribu mambo yote muhimu yanayowahusu wabunge wote bila ubaguzi wa aina yoyote huku akiahidi kuwalinda wabunge wa upinzani walioko Bungeni
“Ndugu zetu wa upinzani mlioko humu ndani mna haki kabisa na moja ya kazi kubwa nikayofanya ni kuhakikisha kwamba na ninyi mnasikika tena vizuri zaidi, lazima tusikike wote.” Ameongeza Spika Ndugai
Amewataka wabunge wasome na kuzifahamu vizuri kanuni, sheria na taratibu mbalimbali za Bunge ambazo zitasaidia kuboresha nidhamu na kusimamia shughuli za kila siku Bungeni
“ Ninaomba sana tusome kanuni na tuzipitie kwa makini na tuzielewe kwa sababu humu ndani hatuwezi kwenda sawa bila kuzijua kanuni kwa hiyo tuzisome, tuzipitie na tuzielewe na baada ya Bunge hili tumeandaa semina ambazo zitatusaidia kutufungua macho na kutusaidia sisi kama wabunge kujua nafasi yetu katika jamii.” Amebainisha Ndugai