Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi leo anatarajiwa kulifungua Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuanza kazi rasmi kwa miaka mitano ijayo.
Taarifa iliyosomwa jana na Spika wa baraza hilo, Zubeir Ali Maulid ilieleza Rais atalizindua baraza leo saa 9 alasiri.
Taarifa hiyo ilieleza kwa mujibu wa utaratibu, baraza hilo ili lianze kazi ni lazima kuzinduliwa na rais baada ya kukamilika kwa baadhi ya shughuli za kikatiba za baraza. Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na kuchaguliwa kwa Spika na Naibu wake.
Kazi nyingine ni kuapishwa kwa wajumbe wa baraza waliohudhuria mkutano huo wakiwemo kutoka majimboni, wa viti maalum pamoja na walioteuliwa na Rais.
Katika kikao cha jana, kulifanyika uchaguzi wa Naibu Spika ambapo wajumbe wote 67 waliohudhuria walimchagua Mgeni Hassan Juma kwa kura zote za ndio.