Serikali ipo mstari wa mbele na itaendelea kutenga fedha na kutoa mchango katika kuziandaa timu za taifa kwa hali na mali hatua ambayo ni kichocheo cha kukuza michezo nchini pamoja na ufadhili unatolewa kwa timu hizo na wadau mbalimbali ndani na nje ya na nchi.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo amebainisha hayo leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi wakati wa hafla ya kuwapongeza wachezaji wa Timu ya mpira wa miguu ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 17 (U-17) ambao ni mabingwa wa michuano Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika, (COSAFA) kwa mwaka 2020/2021.
“Kuanzia sasa kamati zote zitakazokuwa zinahusisha timu za taifa katika michezo yote, wahakikishe Serikali na Baraza zinashiriki tangu mipango ya awali ili kuhakikisha nia ya kusaidia kikamilifu timu za taifa inafanyika hatua itakayosaidia Serikali kufahamu kila kitu kinachoendelea katika michezo yote nchini” Alisema Singo.
Singo ameongeza kuwa ili taifa liweze kufanya vizuri katika michezo ni lazima kuwekeza katika michezo kwa vijana wa chini ya miaka 15, 17, 20 na 23 hatua itakayosaidia taifa kupata timu bora na hatimaye kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali kwa vijana ambao ni uwekezaji wenye tija katika kuandaa timu bora za taifa.
Katika hatua nyingine, Singo amelisisistiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuendelea kushirikiana na vyama vya michezo nchini kuhakikisha michezo husika inakuwa na mchango na kulisaidia taifa kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.
Timu ya ya Taifa ya wanawake ya U-17 wamechukua ubingwa wa michuano Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika, (COSAFA) baada ya kuwafunga Zambia kwenye fainali za mashindano hayo kwa mikwaju ya penati 3-4 kufuatia sare ya 1-1 iliyofanyika uwanja wa Nelson Mandela Bay, Afrika Kusini.
Akiwapokea washindi hao wa COSAFA, Rais waShirikisho la Soka nchini (TFF) Walles Karia amesema ushindi walioupata Timu ya ya Taifa ya wanawake ya U-17 ni zawadi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kwa mlezi wao ambaye pia ni Mkamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan katika kuliongoza taifa.
“Hii imekuwa ni timu ya kwanza kutoa zawadi viongozi wetu, Mhe. Rais na Makamu wa Rais tangu wachaguliwe kuliongoza taifa kwa kipindi kingine cha miaka mitano” alisema Karia
Pia Rais wa TFF amesisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano katika programu za soka zinazotolewa na Shirikisho kwa vijana wa kike na wa kiume kwa kuwa huo ndiyo msingi mzuri wa timu za Taifa kwa miaka ijayo.
Kwa upande wa wachezaji wakiongozwa na Aisha Masaka katika safu ya ufungaji ambaye amekuwa na mchango katika ushindi huo kwa kufunga magoli 10 katika mechi tano ambayo ni wastani wa kufunga magoli mawili kila mechi amesema wameridhishwa na ushirikiano walioupata kutoka Serikalini na viongozi wa TFF hatua iliyowasaidia kufikia kuwa mabingwa wa COSAFA.
Tanzania imekuwa mgeni mwalikwa nchini Afrika Kusini ambaye mara mbili imetwaa kumbe katika ukanda wa COSAFA ambapo mwaka 2019 timu ya U-20 ya wanawake “The Tanzanite” ilialikwa kwenye mashindano hayo ambayo yalifanyika Afrika Kusini ambapo nao walifanikiwa kubeba ubingwa pia.
Wakati huo huo, pia wachezaji wa mchezo wa ngumi za kulipwa Hassan Mwakinyo na Zulfa Yusufu Macho wamepongezwa kwa kupeperusha vema bendera ya taifa kwa kushinda katika mashindano yao yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Zulfa Yusufu Macho alimshinda kwa kwa points Alice Mbewe wa Zambia kwa uzito wa Super Fly weather weight wakati Bondia Mtanzania Hassan Mwakinyo ametetea mkanda wake wa WBF Intercontinental Super Welter Weight baada ya kumtwanga Jose Carlos Paz wa Argentina kwa TKO raundi ya nne.