Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Yohana Budeba akiangalia moja ya mti wa mkorosho uliozalishwa kwa mafanikio makubwa kutokana na mbegu bora zinazozalishwa na Taasisi hiyo kwenye shamba la Kilimo cha Pamoja (Block Farming) eneo la Masigati Wilaya ya Manyoni jana. Budeba kwa kuongozana na wajumbe wa bodi hiyo walifanya ziara ya kukagua kazi zilizofanywa na taasisi hiyo, tija iliyopatikana na kufanya tathmini ya kuona kama kuna haja ya kufanya maboresho zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI nchini, Dkt Geofrey Mkamilo (aliyesimama) akizungumzia mambo kadhaa kuhusu ustawi wa zao la korosho nchini na namna taasisi hiyo ilivyojipanga kuinua tija ya zao hilo katika kuhakikisha malighafi yake inakwenda kutosheleza mahitaji kwenye uchumi wa viwanda, alipofanya ziara kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni kwa kuongozana na Bodi ya Taaasisi hiyo jana.
-Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) wakiwa na baadhi ya wadau na wakulima wa korosho kwenye shamba la Kilimo cha Pamoja, eneo la Masigati, Wilaya ya Manyoni jana, muda mfupi baada ya kukamilisha ziara yao.
Afisa
Kilimo Wilaya ya Manyoni (DIACO), Fadhil Chimsala, akitoa maelezo mbele ya
wajumbe wa Bodi ya TARI ya namna wanavyoshirikisha wadau mbalimbali (wakiwemo
Jeshi la Magereza) katika kuzalisha miche ya mbegu bora zinatoka Kituo cha
Utafiti TARI-Naliendele na kuzisambaza kwa wakulima wakati wa ziara ya wajumbe
wa Bodi hiyo kwenye Gereza la Manyoni jana.
Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Naliendele, Dkt Fortunatus Kapinga akitoa maelezo kwa wajumbe wa Bodi ya namna taasisi hiyo ilivyojipanga kuzalisha mbegu za korosho za kutosheleza mikoa yote ya Kanda ya Kati, sambamba na kuwaonyesha maandalizi ya awali na ukubwa wa shamba hilo la mfano lenye takribani ekari 30, lililopo Masigati, Manyoni jana.
- Mkurugenzi
wa Kituo cha TARI Naliendele, Dkt Fortunatus Kapinga akiendelea kutoa maelezo
ya kitaalamu kuhusu mwendelezo na tija ya shamba hilo litakaloanza kuzalisha mbegu
bora za korosho.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt Mkamilo akieleza namna Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ilivyojipanga kuongeza tija ya zao la Korosho sambamba na kuchangia ustawi wa viwanda nchini.
Na Godwin Myovela, Singida
BODI ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) imetoa wito kwa watafiti wake sambamba na wadau wa taasisi hiyo kuhakikisha wanaongeza kasi zaidi katika kuleta mapinduzi ya kilimo katika muktadha wa shabaha ya kuongeza malighafi ya kutosha kwenye ukuaji wa viwanda vya ndani, na kubadilisha kwa pamoja mfumo mzima wa kilimo kutoka kile cha kujikimu kwenda cha kibiashara
Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Dkt Yohana Budeba aliyasema hayo eneo la Masigati, Wilaya ya Manyoni, mkoani hapa jana, eneo unapotekelezwa mradi wa ‘Kilimo cha Pamoja’ cha zao la Korosho, alipotembelea na kuangalia sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya bodi kwa taasisi yake
Budeba mbali ya kupongeza dhamiri ya dhati ya Rais John Magufuli katika mantiki ya kuinua tija ya kilimo nchini kupitia hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la 12, aliwataka watafiti na wadau wengine wa kilimo kuunga mkono juhudi za serikali ili kuchagiza kasi ya mabadiliko hayo, sanjari na kusukuma ukuaji wa uchumi.
“Kwa mujibu wa Rais Magufuli serikali imedhamiria kuongeza juhudi ili kubadilisha kilimo cha Tanzania kuwa cha kibiashara. Hivyo ni jukumu letu watafiti na wakulima kwenda pamoja na dhamiri hiyo njema ili kuongeza tija,” alisema Budeba
Alisema katika kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na maelekezo ya serikali, Bodi yake imefarijika sana kuona maagizo iliyotoa ya kuhakikisha ugunduzi na teknolojia zote zinawafikia walengwa limezingatiwa na kutekelezwa mpaka sasa kikamilifu
Baadhi ya maagizo yaliyotolewa na bodi hiyo inayoundwa nawajumbe 12 kutoka taasisi na wadau mbalimbali na utekelezaji wake, ilikuwa ni kuitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo kuhakikisha inasambaza kwa kasi teknolojia zake hususani eneo la ugunduzi wa mbegu bora kwa tija ya mkulima na ustawi wa kilimo nchini-jambo ambalo limeendelea kutekelezwa kwa ukamilifu.
Agizo lingine lilikuwa ni kuitaka TARI kufanya tafiti yenye lengo la kupanua wigo wa kilimo cha zao la korosho kutoka mikoa 5 iliyokuwa ikilima zao hilo, jambo ambalo nalo limetekelezwa ipasavyo kwa taasisi hiyo mpaka sasa kufanikisha kwa tija uanzishwaji wa kilimo cha zao hilo kwa mikoa takribani 20 ikiwemo Singida, ambayo alipongeza kwa kuendelea kufanya vizuri hususan kupitia shamba lake la masigati lenye takribani ekari elfu 22 zinazolimwa zao hilo kwa tija na mafanikio makubwa
Budeba aliwataka wadau wa sekta za umma na binafsi yakiwemo Majeshi na Amcos za kilimo kushirikiana na TARI katika kupanua wigo wa usambazaji wa teknolojia zake kwa kasi na tija ili ziweze kufikia idadi kubwa zaidi ya wakulima kwa haraka
“Kuona ni kuamini..nawasihi watanzania watembelee shamba hili la Masigati ili wajifunze teknolojia hizi tunazozizalisha. Pia tunakaribisha mashirikiano na sekta nyingine, mathalani Jeshi la Magereza wao wamekwishaanza, shabaha yetu ni kuzalisha kwa tija ili kuondokana na kilimo cha kujikimu,” alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI nchini, Dkt Geofrey Mkamilo, alisema hitaji la Taasisi hiyo kwa sasa ni kuona uzalishaji wa teknolojia zake, ubunifu na mbinu bora za kilimo zinakwenda sambamba na ukuaji wa viwanda-huku taasisi ikiahidi kuongeza juhudi katika kuhakikisha kiwango cha asilimia 60 za malighafi ya kilimo kwenye viwanda vya ndani na zaidi ya hapo inafikiwa ipasavyo.
Alisema pamoja na mambo mengine, shabaha iliyopo mbali ya kupanua wigo wa huduma za kiugani kwa kushirikiana na wadau, taasisi imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbegu za korosho ili kukidhi mahitaji ya mikoa yote 20 inayolima zao hilo, na stratejia iliyopo ni kuzalisha kutoka wastani wa tani takribani laki 3 zinazozalishwa kwa sasa kufikia tani milioni 1 ifikapo 2024.
“Maono ya Rais Magufuli ni kuona tija inaongezeka zaidi kupitia hasa mazao haya ya kimkakati likiwemo zao la korosho. Na katika hili tumejipanga vizuri kuhakikisha tunakwenda kuzalisha mabilionea wa kutosha kupitia takribani mazao yote 85 ikiwemo korosho tunayoshughulika nayo, lengo ni kumtoa mkulima kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kile cha kibiashara” alisema Mkamilo.