Na Calvin Edward Gwabara, Morogoro
UTAFITI uliyofanywa na Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) umebainisha kuwa usawa wa kijinsia unaimarika na kuzingatiwa sana kwenye vijiji vinavyoshiriki miradi ya uhifadhi shirikishi wa Misitu kupitia Shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania -TFCG.
Hayo yamebainika na Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyama pori na utalii Profesa. Suzan Augustino wakati wa uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti mbele ya wadau wa misitu mjini Morogoro na kusema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na TFCG na Mtandao wa Jamii wa usimaizi wa Misitu Tanzania MJUMITA kwa kuhakikisha jamii yote inashirikishwa na inanufaika na rasilimali zitokanazo na misitu hiyo.
“ Kuna mabadiliko makubwa chanya kwenye vijiji ambavyo TFCG na MJUMITA wanatekeleza miradi yao hasa wa mkaa endelevu ikilinganishwa na vijiji vilivyo nje ya mradi ingawa wanaume wanaongoza kwenye kazi zinazohitaji nguvu” alibainisha Prof. Suzan.
Prof. Suzan alisema kuwa kwenye Mradi wa Mkaa Endelevu wanawake wanakuja juu katika kushiriki kwenye biashara hiyo ijapokuwa wao wanatumia fedha kulipa watu kufanya kazi zao kama vile kukata magogo, kuyakusanya na kupanga tanuri la mkaa kazi ambazo zinaonekana kuhitaji nguvu zaidi.
Aidha Suzan alisema kuwa baadhi ya vijiji vina ushiriki mdogo wa wanawake na hiyo kwa mujibu wa utafiti wao wamesema inasababishwa mila na destuli Zao kwamba kazi za maporini hufanywa na wanaume tu na sio wanawake ingawa mitazamo hiyo imeanza kufutika taratibu baada ya jitihada za TFCG na MJUMITA za kutoa elimu.
Prof. Suzan alisema watu wengi wanajua usawa wa kijinsia kwenye ngazi za maamuzi ni kuwa na idadi sawa ya wanawake, wanaume na Makundi mengine lakini ukweli ni kwamba kinachotakiwa kuangaliwa ni nani kawakikisha kundi gani na sauti ya like na mchango wake kwenye kufanya maamuzi maana wanaweza kuwa idadi sawa lakini wote hawana sauti.
Kwa upande wake Prof. John Jackoniah Mtafiti kutoka Ndaki ya Sayansi za jamii na Insia - SUA alisema pamoja na mafanikio hayo ya kuongeza uwiano wa kijinsia kwenye jitihada za usimamizi shirikishi wa Misitu na matumizi ya mapato ya rasilimali hizo lakini wanaume ndio wameonekana kunufaika zaidi.
Alisema kupitia utafiti huo walioufanya kwenye vijiji 10 katika Wilaya za Kilosa, Mvonero na Morogoro wanaume ndio wameonekana kuwa na sauti zaidi kwenye maamuzi na hata kwenye kugawana rasilimali za misitu kwenye maeneo hayo.
“ Lakini utaona wanawake walioolewa ndio wasio na sauti zaidi lakini wale ambao hawajaolewa au waliopewa talaka wananufaika Kama wanaume na Pia wana sauti kwenye kutoa maamuzi na kwenye kugawana mapato ya rasilimali za Misitu” alifafanua Prof. Jackoniah.
Alisema kuwa ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za kibiashara za rasilimali za Misitu umeongeza mzigo kwa wanawake kwakuwa kazi za nyumbani nazo zinawaangalia kwakuwa mgawanyo wa majukumu ya nyumbani haujabadilika umebaki palepale.
Akieleza lengo la Utafiti huo Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema masuala ya kijinsia yametengenezewa mkakati mahususi wa kuhakikisha yanazingatiwa kikamilifu kwakuwa ni swala mtambuka kwenye maendeleo.
Alisema baada ya kutekeleza Mradi kwa muda sasa wameona wafanye Utafiti huo ili kuona namna maswala hayo yanavyozingatiwa na kutafuta njia za kuboresha zaidi kama kuna vitu Vinakosekana kupitia mapendekezo ya watafiti hao kutoka SUA.
Social Plugin