Rais Donald Trump wa Marekani amesema kwa mara ya kwanza kwamba ataondoka ikulu ya White House iwapo rais mteule Joe Biden atathibitishwa rasmi kuwa mshindi wa uchaguzi wa Marekani.
Hata hivyo Trump bado anaendeleza madai yake kwamba uchaguzi huo kuvurugwa.
Trump alifanya majaribio kadhaa ambayo hayakutarajiwa ya kuyakataa matokeo ya uchaguzi kwa kukataa kukubali kushindwa, huku akiibua nadharia kadha wa kadha kuhusu kuibiwa kura na hata kufungua madai yasiyo na uthibitisho mahakamani, ambayo hata hivyo yalitupiliwa mbali na mahakama za Marekani.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari tangu uchaguzi wa Novemba 3, rais Trump alionekana kukaribia kukubali kwamba atahudumu kwa muhula mmoja kabla ya Biden kuapishwa Januari 20 mwakani.
Na baada ya kuulizwa iwapo ataondoka White House, kama jopo la wajumbe maalumu wa uchaguzi la Electoral College litauthibitisha ushindi wa Biden, Trump alikubali kwamba ataondoka na kuongeza kuwa hata waandishi hao wa habari wanajua kwamba ataondoka.