WATU WATANO WATEKETEA KWA MOTO BAADA YA MAGARI MAWILI KUGONGANA TANGA


Magari yakiteketea baada ya kugongana mkoani Tanga.
Watu watano wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 21, 2020, mara baada ya malori mawili kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Kitumbi wilayani Handeni mkoani Tanga, huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni uzembe wa kutokuzingatia sheria za usalama barabarani.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga ACP Blasius Chatanda, amesema kuwa malori hayo moja lilikuwa likitokea jijini Dar es Salaam likiwa na vifaa vya dukani likielekea mkoani Tanga, na lingine lilikuwa limebeba saruji kuelekea mkoani Dodoma.

"Gari mbili zimewaka moto ni wazi kwamba magari yote haya mawili yalikuwa kwenye mwendokasi, kwa mujibu wa mashuhuda gari moja ilihama kutoka upande wake na ku-overtake gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na kugongana, hiyo miili ilivyo ni ngumu hata kufanya utambuzi kwa sababu wameungua vibaya na miili yote imehifadhiwa kwenye kituo cha afya Mkata", amesema ACP Chatanda.

Aidha ACP Chatanda, akatoa rai kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, kwa sababu huo ni mwarobaini wa ajali zote za barabarani.

CHANZO - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post