Polisi nchini Uganda imethibitisha vifo vya watu watatu kutokana na machafuko yaliyozuka alasiri ya Jumatano kufuatia habari za kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine
Machafuko hayo yalisambaa katika miji kadhaa na kusababisha watu wengi kujeruhiwa kutokana na risasi na mabomu ya kutoa machozi. Hii imewalazimu wagombea wawili kwa kiti cha urais kusitisha kampeni zao hadi pale mwenzao atakapoachiwa.
Wagombea hao wamesema ni vigumu kwao kuendelea na kampeni huku mgombea mwingine akiwa anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi.
Bobi Wine alikamatwa jana Jumatano Mashariki mwa eneo la Luuka baada ya polisi kumshtumu kwa kosa la kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliowekwa na Tume ya Uchaguzi.
Na punde tu baada ya wafuasi wake kupata taarifa, walianza kuandamana wakidai aachiliwe huru. Mgombea mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia amekamatwa.