ASKOFU SANGU ATUMA SALAMU SIKUKUU YA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2021..."ASISITIZA KUTENDA MEMA ZAIDI"


Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Liberatus Sangu

Na Damian Masyenene- Shinyanga 
Desemba 25 kila mwaka, Wakristo kote duniani huungana katika kuadhimisha sikukuu ya Noeli kuzaliwa kwa mwokozi wao Yesu Kristo (Christmas), ambapo kuelekea siku hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Liberatus Sangu amewatumia salamu za Sikukuu ya Krismasi waumini wa kanisa hilo na kuwataka kuisherehekea nyumbani na watoto kwa kudumisha utulivu na usalama wakiepuka vitendo vya kihalifu.

Askofu Sangu ametoa salamu hizo leo Desemba 24, 2020 katika ofisi zake Ngokolo mjini Shinyanga ikiwa ni maandalizi ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi, huku akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo mengi aliyowatendea wanadamu kwa mwaka mzima 2020 licha ya mapungufu mbalimbali waliyonayo wanadamu. 

"Ndugu zangu tunaingia katika kipindi kitakatifu cha kufanya tafakari kuhusu kuzaliwa mwokozi wetu Yesu Kristo, yaani maadhimisho ya Sikukuu ya Noeli au Christmas. Maadhimisho haya ni fursa muhimu ambayo iliwekwa na Kanisa kutoa nafasi ya pekee kutafakari kwa kina fungu la ukombozi kwa mwanadamu baada ya mahusiano yake na Mungu kulegalega.

"Katika kusherehekea sikukuu za Christmas na mwaka mpya 2021 tusherehekee kwa amani na utulivu, suala la usalama wetu na familia zetu tulipe kipaumbele, tusherehekee sikukuu hizi kwa pamoja na watoto wetu tusiwaache wazurure hovyo mitaani na kwenye kumbi za starehe……tutumie fursa ya sikukuu hizi katika kutenda mema zaidi na kuepuka vitendo vya kiharifu," amesema Askofu Sangu.

Sangu amewasihi wakristo kuendelea kuomba neema za Mwenyezi Mungu ili azidi kuwatia nguvu, huku akimshukuru Mungu kwa namna ambavyo ameiwezesha nchi ya Tanzania kumaliza salama zoezi la uchaguzi mkuu na janga la Corona, na kueleza kuwa kwa sasa kilichobaki ni kuendelea kushirikiana ili kuijenga nchi.

"Wapendwa wanafamilia ya Mungu, tunapoadhimisha fumbo hili pia tunaingia katika kipindi kingine cha mwaka mpya 2021 kwa namna ya pekee tunapaswa kumrudishia Mungu sifa, shukurani na utukufu kwa mema mengi aliyotujalia kwa mwaka 2020 na kuomba Baraka kwa mwaka mpya 2021," amesisitiza. 

KUDUMISHA AMANI, KUKEMEA CHUKI 
Askofu Sangu ametumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania kudumisha amani ya nchi, huku akiwataka wanasiasa kutokuwa chanzo cha kuvuruga na kugawa wananchi kwa kauli za kuchochea chuki.

"Nitumie nafasi hii kuwaomba Watanzania wote popote pale tulipo kila mmoja kwa nafasi yake kutokubali kuipoteza amani tuliyonayo, tusikubali mtu yeyote asiichezee tunu hii, na tutambue kuwa Tanzania ikichafuka hakuna mahali popote pa kukimbilia. Kila mmoja wetu awe himbuko la amani, faraja, furaha, na upendo. 

"Niwaombe ndugu zangu wanasiasa tuepukeni mambo yote ambayo yanaweza kuhatarisha amani ya nchi, tuepuke kutoa matamshi ya chuki ya kutugawa na kuvunja Umoja na mshikamano wetu na badala yake tutamke na kufanya matendo ambayo yatatuunganisha kwa pamoja kama Watanzania," ameeleza Askofu Sangu 

Pia Askofu Sangu amewahimiza wanasiasa kutafuta maridhiano na kumaliza tofauti zao ndani ya nchi pale wanaposhindwa kuelewana, huku akieleza kuwa kukimbilia nje ya nchi kutafuta maridhiano ni utumwa na fedheha kwani watu wabaya wanaweza kuitumia fursa hiyo kuvuruga amani ya nchi.

"Natoa wito kwa wanasiasa pale tunapotofautiana tujitahidi kupata ujasiri wa kukutana na kufanya maridhiano ya kumaliza tofauti zetu haraka hapa hapa ndani ya nchi badala ya kuvuka ng’ambo hatua ambayo inaweza kutumiwa kama fursa na watu ambao hawaitakii mema Tanzania," amesema. 

VITENDO VYA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO 
Katika kuhakikisha vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa watoto na wanawake vinatokomezwa, Askofu Sangu ameiomba jamii kuungana kwa pamoja kukemea vitendo hivyo huku akitoa wito kwa wasimamizi wa fedha za wahisani zinatolewa kwa ajili ya kupambana na vitendo hivyo zinatumika ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta matokeo chanya.

"Bado kuna idadi kubwa ya matukio ya ukatili mikoa ya Shinyanga na Simiyu, kuendelea kuwepo kwa vitendo vya mauaji ya wanawake kutokana na imani za kishirikina, wanawake wajane kuendelea kunyanyaswa na kunyang’anywa urithi, wanaume kutowajibika katika malezi ya familia, watoto wa kike kukatishwa masomo kwa mimba za utotoni na kuozeshwa katika umri mdogo. 

"Nitumie nafasi hii kuwaomba tuungane kwa pamoja kukomesha mambo haya ili tupate maendeleo, hatuwezi kupata kuendelea kama mambo haya yanatokea, tusikubali kuendelea kuona watoto na wanawake wananyanyasika," amesisitiza. 

CHANZO - SHINYANGA PRESS CLUB BLOG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post