Na Dinna Maningo,Tarime
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoani Mara Apoo Tindwa ameahidi kutoa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Nyamwaga kata ya Nyamwaga.
Tindwa ametoa ahadi hiyo leo baada ya Wanafunzi wa kike kumuomba mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara kuwapatia msaada wa taulo za kike wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule hiyo.
"Changamoto zingine ziko ndani ya uwezo wa mbunge ila hili la taulo za kike liko ndani ya uwezo wangu nawahaidi januari,2021shule zikifunguliwa nitawanunulia hizo taulo ondoeni shaka", alisema Tindwa.
Elizabeth Boniface ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo alisema kuwa endapo watapata taulo za kike zitawasaidia kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanatoka katika familia zisizo na uwezo ambazo haziwezi kutoa fedha za kununua taulo za kike.
Mkuu wa shule hiyo Mwita Nyambacha alisema shule ina wasichana 196 nakwamba Serikali imetoa milioni 80 kujenga Bweni la wasichana ambalo ujenzi umefikia hatua ya msingi.
"Bweni hilo litachukua wanafunzi 80,ujenzi umechelewa kutokana na ubovu wa barabara baada ya mvua kunyesha na kusababisha gari kushindwa kufika kutuletea vifaa kama saruji,mchanga barabara haipitiki,bweni hili likikamilika litasaidia wanafunzi wanaotoka mbali", alisema Nyambacha.
Hata hivyo Waitara aliwataka wananchi na kamati inayosimamia ujenzi kuhakikisha hakuna ubadhilifu wa fedha na majengo yajengwe kwa kiwango kinachohitajika nakwamba wale watakaoboronga kazi wasipewe kazi nyingine.