Rais Dk. John Pombe Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amesema atafanya uteuzi wa naibu waziri mwingine wa Madini baada ya aliyemteua, Francis Ndulane Kumba ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini kushindwa kuapa leo Jumatano Desemba 9, 2020 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Ndulane ambaye ni mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM) mwenye elimu ya shahada ya uzamili alikuwa mmoja wa waliotakiwa kuapa lakini ameshindwa kusoma kiapo mbele ya Rais Magufuli, akikosea mara kadhaa kila alipopewa nafasi ya kurudia kusoma na ndipo katibu mkuu kiongozi, John Kijazi kumtaka aende kuketi kwanza ili wenzake waendelee kuapa.
"Kila mmoja nimemuangalia mpaka wewe uliyeshindwa kuapa.
Tutamteua mtu mwingine anayeweza kuapa vizuri",amesema Rais Magufuli.
Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge, Ndulane ana elimu ya shahada ya uzamili katika uhasibu na fedha ambayo ameisomea katika Chuo Kikuu cha Mzumbe kati ya mwaka 2013 na 2015. Pia, ana stashahada ya juu ya uhasibu kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM).
Ndulani alisoma shule ya msingi Uwanjani (mwaka 1980 - 1986), baadaye akaenda sekondari ya Tambaza (mwaka 1987 - 1990) na baada ya kuhitimu kidato cha nne, alikwenda sekondari ya Pugu (mwaka 1991 - 1993).
Social Plugin