MUAROBAINI LISHE DUNI SINGIDA WAPATIKANA

Na Abby Nkungu, Singida
TATIZO la utapiamlo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano huenda likabaki kuwa historia katika baadhi ya maeneo mkoani Singida baada ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kuanzisha mradi wa Boresha Lishe katika vijiji 85 vya wilaya za Ikungi na Singida.

Meneja Mkuu wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Mpango Endelevu wa Uboreshaji Mazingira (SEMA) la mjini Singida linalotekeleza mradi huo, Ivo Manyaku, alisema wamejikita zaidi katika kutoa mafunzo ya kilimo bora cha uzalishaji mboga, matunda na ufugaji wa wanyama wadogo ili kuboresha lishe ngazi ya familia.

“Kumekuwepo na tatizo la utapiamlo katika mkoa wetu na moja ya sababu ikitajwa kuwa wanaume, ambao ndio watoa maamuzi ya fedha kwenye familia, hawaendi kliniki na wenzi wao wakiwa wajawazito ili kwenda kupewa elimu ya lishe bora kwa mama na mtoto” alisema na kuongeza;

Aidha, baadhi ya ripoti za kiutafiti na taarifa kupitia vyombo vya habari, zinadai kuwa kutokana na wanaume kutojua umuhimu wa lishe bora huwa hawaoni sababu ya kutenga fedha kwa ajili ya lishe bora kwa mama na mtoto hali inayochangia kuwepo utapiamlo, udumavu na uzito pungufu kwa watoto".

Alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo, mradi huo unaotekelezwa kwa kushirikiana na RECODA, umekuwa mkombozi kwa kuwa unawafikia wanafamilia wote kwenye maeneo yao ya vijijini na kuwapa elimu ya lishe bora; namna ya kuanzisha bustani za mboga, matunda na kufuga wanyama wadogo. 

Alisema kuwa njia hii imekuwa rahisi zaidi katika kuwafikia akina baba vijijini badala ya kuwasubiri waambatane na wenzi wao siku ya Kiliniki; hivyo kuleta ufanisi katika kupunguza udumavu, utapiamlo na uzito pungufu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupitia mkoba wa siku 1000. 

Alisema kuwa hadi hivi sasa jumla ya bustani za nyumbani 9,590 zimeanzishwa Wilayani Singida na nyingine 7,704 Ikungi zikiwa zimelimwa mboga na matunda baada ya wananchi kupatiwa elimu na mbegu za beetroot, viazi damu, chinese, spinachi, mnafu na miti ya mipapai, miembe na mipasheni; nyingi ya bustani hizo zikiwa zimeanzishwa na kusimamiwa na wanaume.

Ofisa Lishe Mkoa, Bi Teda Sinde ameshukuru kuanzishwa kwa mradi huo huku akiomba usambazwe vijiji vyote akisema kuwa vyakula hivyo ni muhimu na iwapo wananchi watazingatia matumizi yake; hasa kwa wajawazito na watoto tatizo la utapiamlo, udumuvu na uzito pungufu kwa watoto litabaki kuwa historia.

Takwimu za utafiti wa kitaifa za mwaka 2018 juu ya hali ya lishe mkoani Singida zinaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo.

Kadhalika, utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia 3 tu ya watoto walio chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post