Na Grace Mwakasendile Mbeya
Mhubiri wa Kimataifa wa Injili kutoka nchini Marekani, Donna Molley amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Poombe Magufuli kwa ujasiri wake wa kupambana na Ugonjwa wa Covid – 19 unaosababishwa na maambukizi ya Virusi vya Corona akieleza kwamba ni kiongozi wa kwanza duniani ambaye amemshikirisha Mungu katika mapambano ya ugonjwa huo.
Mhubiri wa Kimataifa wa Injili kutoka nchini Marekani, Donna Molley ametoa pongezi hizo akiwa mkoani Mbeya baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, kwa ajili ya kuhubiri kwenye mkutano mkuu wa injili ambayo utafanyika kwa siku 4 mfululizo kwenye uwanja Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.
Amesema Rais Dk. Magufuli ni mfano wa kuigwa kutokana na utendaji kazi wake pamoja na imani aliyonayo katika kumtegemea Mungu na kushinda katika vita dhidi ya ugonjwa wa Covid 19.
Naye profesa Donald Mwanjoka ambaye ni Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste katika Mkoa wa Mbeya amemtaja Rais Dk. Magufuli kuwa ni kiongozi ambaye anamshirikisha Mungu katika kila hatua za uongozi wake.
Ameahidi yeye na viongozi wengine wa dini kuendelea kumuombea na kumpa ushirikiano katika kila jambo analolifanya ili kuliletea maendeleo taifa la Tanzania.
Mkutano Mkuu wa Injili unatarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 10 hadi 13 ukitanguliwa na kongamano la Wanawake, ambapo wagonjwa mbalimbali wataombewa wakiwemo wenye mahitaji maalum.