RAIS MAGUFULI AMTEUA PROF. MANYA KUJAZA NAFASI YA ALIYESHINDWA KUAPA.... ATAAPISHWA LEO LEO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Shukrani Manya kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Madini na ataapishwa leo mchana Ikulu Chamwino Dodoma.


Disemba 9,2020 Rais Magufuli alisema atafanya uteuzi wa Naibu Waziri mwingine wa Madini baada ya aliyemteua, Francis Ndulane Kumba ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini kushindwa kuapa Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. 

Ndulane ambaye ni mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM) mwenye elimu ya shahada ya uzamili alikuwa mmoja wa waliotakiwa kuapa lakini alishindwa kusoma kiapo mbele ya Rais Magufuli, akikosea mara kadhaa kila alipopewa nafasi ya kurudia kusoma na ndipo katibu mkuu kiongozi, John Kijazi kumtaka aende kuketi kwanza ili wenzake waendelee kuapa.

 Ndulane alisitasita na kukosea, kurudia hadi alipokatizwa na kutakiwa kupumzika.

“Mimi Francis Kumba Ndulane naapa kwamba,” akasimama kwa muda na kuendelea “nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, kabla ya kusimama tena kwa muda na kuanza upya kusoma kiapo kwa kasi kidogo.

“Mimi Francis Kumba Ndulane naapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba,” anasimama tena na kuinamia zaidi karatasi yenye kiapo ili kusoma vizuri kabla ya kukkiinua juu na kusogeza usoni na kuanza tena kusoma.

“Mimi Francis Kumba Ndulane naapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba nitaihifadhi, nitailinda na kuitetea Katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria iliyowekwa. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie.”

Alisoma sehemu ya pili ya kiapo hicho kwa kutetereka tena na alipomaliza, Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi alimtaka arudie tena kusoma kiapo.

Safari ya pili alisita zaidi hadi walipomkatisha na kumtaka arudi kupumzika.

Ndulane ana elimu ya shahada ya uzamili katika uhasibu na fedha ambayo aliipata Chuo Kikuu cha Mzumbe kati ya mwaka 2013 na 2015. Pia, ana stashahada ya juu ya uhasibu kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM).

Ndulane alisoma shule ya msingi Uwanjani (mwaka 1980 - 1986), baadaye akaenda sekondari ya Tambaza (mwaka 1987 - 1990) na baada ya kuhitimu kidato cha nne, alikwenda sekondari ya Pugu (mwaka 1991 - 1993) ambako alihitimu kidato cha sita.

Ili kupata shahada ya uzamili, Ndulane aliandika chapisho kuhusu changamoto wanazopata makandarasi wadogo na wa kati na kuathiri utendaji wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post