Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Jenipher Mahesa
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mamia ya
wakazi wa Shinyanga na maeneo jirani wamejitokeza kwenye Mazishi ya Mwandishi
wa Habari na Mtangazaji wa Redio Faraja Fm Stereo Jenipher Mahesa (32)
aliyefariki dunia siku ya Ijumaa Disemba 4,2020 wakati akipatiwa matibabu
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Jenipher
Mahesa amefariki dunia wakati akipata matibabu baada ya kupata ugonjwa wa
kupooza tangu tarehe 5.7.2020 na kutibiwa katika hospitali mbalimbali lakini
hali yake ilibadilika zaidi tarehe 23.11.2020 na kupelekea kifo chake tarehe 4.12.2020.
Mazishi ya marehemu Jenipher Mahesa yamefanyika leo Jumamosi Disemba 5,2020 jioni katika makaburi ya Dodoma yaliyopo kata ya Ndembezi Mjini Shinyanga.
Akitoa
salamu za rambirambi, Mkurugenzi wa Redio Faraja Padre Anatoly Salawa amesema
Redio Faraja na Kanisa Katoliki limepoteza mfanyakazi mchapakazi aliyeipenda
sana kazi yake akieleza kuwa Jenipher alikuwa Mwandishi Mahiri wa Habari na aliyebobea katika
vipindi vya dini.
“Jenipher
Mahesa alikuwa mfanyakazi mchapakazi sana. Anatambulika kwa umahiri wake mkubwa
katika habari na utangazaji wa vipindi vya dini. Tumeondokewa na nguvu kazi
kubwa, Jenipher aliipenda sana Radio Faraja”,amesema Padre Salawa.
“Kupitia kazi yake kama mwanahabari amewaelimisha wana Shinyanga, amewaburudisha kupitia
kazi yake ya uandishi wa habari, amekuwa mpishi mzuri wa habari, mchango wake ni mkubwa sana kama
mwanahabari. Msiba huu siyo wa Radio Faraja tu bali ni kwa watu wote wanaomfahamu na wanaotambua kazi zake”,ameongeza Padre Salawa.
Naye Katibu
Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari (Shinyanga Press Club – SPC) , Kosta
Kasisi amesema Jenipher alikuwa mwanachama wa SPC wa pekee sana kutokana na
upole, upendo, nidhamu na unyenyekevu kwa waandishi wa habari wenzake na wadau
wa habari.
Naye
Mwenyekiti wa mtaa wa Dome kata ya Ndembezi, Solomon Nalinga Najulwa amesema
Jenipher Mahesa alikuwa ni
mtu aliyejitoa sana katika masuala ya kijamii na alikuwa mstari wa mbele kupigania
masuala ya haki za watoto na wanawake.
Jenipher Paul Mahesa alizaliwa tarehe 23.3.1988 amefariki dunia tarehe 4.12.2020, ameacha watoto wawili wadogo wa kike.
Social Plugin