Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GELARD NG'ONG'A ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA RORYA MARA

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a akila kiapo cha utii kwa mujibu wa sheria na kanuni mara baada ya kuchaguliwa kuwa diwani wa kata ya Rabour wilayani Rorya. 

Na Suleiman Abeid, Rorya 
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, mkoani Mara limemchagua diwani wa kata ya Rabour, Gerald Samwel Ng’ong’a kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikichukuliwa na diwani Oresi Simba. 

Kwa mujibu wa matokeo ambayo yametangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi huo, Murumbe Daudi, Ng’ong’a amechaguliwa kuwa Mwenyekiti baada ya kupata kura zote 35 za ndiyo baada ya mpinzani wake kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, Khalfan Abdul kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho. 

“Naomba nitangaze matokeo ya uchaguzi wetu ambao umefanyika katika hali ya amani na utulivu na kwa uwazi. Wapiga kura walikuwa ni 35, kura za ndiyo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri zilikuwa ni 35, hakuna kura ya hapana,” 

“Hivyo kwa Mamlaka na kanuni, natamka rasmi kwamba Mheshimiwa, Gerald Ng’ong’a ndiye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, na nafasi ya Makamu mwenyekiti wapiga kura walikuwa 35, pia hakuna kura iliyoharibika, kura za ndiyo zilikuwa 35 hakuna kura ya hapana, natamka rasmi kwamba Makamu mwenyekiti ni Bwana Oresi Simba,” ameeleza Daudi. 

Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Mwenyekiti mpya na Makamu wake walipata fursa ya kutoa shukrani zao kwa madiwani waliowachagua ambapo kwa upande wake, Mwenyekiti Ng’onga mbali ya shukrani pia alieleza vipaumbele vyake katika kuitumikia Halmashauri hiyo ya Rorya. 

Moja ya vipaumbele ambavyo vimeanishwa na Mwenyekiti huyo ni pamoja na suala la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ambapo amesema katika kipindi chake chote cha uongozi atahakikisha suala la usimamizi wa mapato analisimamia kwa ukaribu ili kuwezesha ongezeko la mapato ya ndani na hivyo kuwaeletea wananchi wa Rorya maendeleo waliyoahidiwa kipindi cha kampeni. 

“Wapiga kura wote 35 mlioshiriki katika zoezi la kumchagua Mwenyekiti mmekuwa na imani kubwa sana kwangu na ndiyo maana kura zote zimepigwa kwangu kwa uaminifu na kwa imani, nasema ahsanteni sana kwa imani hiyo,” 

“Na mimi nimeipokea imani hiyo na kwangu mimi sasa nina wajibu wa kuonesha utii na nidhamu na kuwatumikia kwa mujibu wa imani hiyo, lakini pia niwapongeze wenzangu kutoka upande wa pili kwa busara zao za kuniachia mimi niweze kuendelea, mheshimiwa uliyeniachia nafasi nakushukuru kwa heshima ya kipekee,” anaeleza Ng’ong’a. 

Kwa upande mwingine, Ng’ong’a ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki Social Development Organization – Rafiki SDO lenye makao yake makuu mkoani Shinyanga, amewaomba madiwani wenzake wampatie ushirikiano wa dhati katika kufanya kazi. 

Amesema kwa sasa uchaguzi umekamilika na kazi iliyopo mbele yao ni kuchapa kazi na kwamba hawatoweza kufanya kazi kwa usahihi iwapo hapatokuwepo ushirikiano miongoni mwao na kwamba wanachokitarajia ni kuona maendeleo yakipatikana katika Halmashauri yao na si malumbano ya kisiasa. 

“Madiwani wote mliopo hapa, mabwana na mabibi kwa kilichotendeka ni dhahiri kwamba uchaguzi sasa tumemaliza kilichobaki sasa tuchape kazi, tunajiandaa kufanya kazi lakini hatuwezi kufanya kazi iwapo hatutashirikiana,” anaeleza Ng’ong’a. 

Amewaomba madiwani hao washirikiane katika suala zima la usimamizi wa mapato ya Halmashauri kwa vile ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo yote yanayotarajiwa kutekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Rorya. 

Amesema kuanzi sasa ni vizuri mapato yote yakakusanywa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki badala ya kukusanywa kwa stakabadhi za karatasi mapato yote hata katika maeneo ya minada yote yakusanywa kwa mfumo huo badala ya mtumishi kukusanya fedha taslimu kutoka wa wafanyabiashara. 

“Jambo la pili nikuombe Mkurugenzi kuanzia sasa malipo yote vikao vya madiwani yaanze kupitia kwenye akaunti zao za Benki, madiwani wote wawasilishe akaunti zao benki ili posho zao zilipwe kupitia benki hata kama ni posho ya shilingi elfu kumi, akutane nayo benki, hili ni suala la muhimu sana,” anaeleza Ng’ong’a. 

Awali wakati zoezi la uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo likianza, Msimamizi wa uchaguzi huo alitangaza kupokea majina ya wagombea wawili kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Gerald Ng’ong’a na Chama cha ACT-Wazalendo, Khalfan Abdul. 

Hata hivyo mara baada ya mgombea wa ACT-Wazalendo kupewa nafasi ya kuomba kura kwa madiwani alitangaza rasmi kuondoa jina lake katika kinyang’anyiro hicho kwa madai ya kuamini kwamba mpinzani wake kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ana uwezo mkubwa wa kuitumikia nafasi hiyo. 

"Ndugu madiwani nimesimama hapa bila ya kushawishiwa na mtu ye yote na kwa hiari yangu mwenyewe, nikiwa na akili timamu ninasema kwamba ninaomba kujiondoa kwenye kugombea nafasi hii ya uenyekiti na kumwachia mgombea wa CCM, Gerald Ng'ong'a ambaye ni diwani mwenzangu kutoka kata ya Rabuor. 

“Naamini yeye anatosha na ana uwezo mkubwa wa kutuongoza sisi madiwani wenzake ili tuweze kuiletea maendeleo ya kweli Halmashauri yetu ya wilaya ya Rorya kama tulivyowaahidi wananchi kipindi cha kampeni za kuomba kura, na tukumbuke suala la maendeleo halina vyama,” anaeleza Abdul. 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a (kushoto) na Makamu wake Oresi Simba (kulia) wakivaa rasmi majoho yao kabla ya kuanza kuendesha kikao cha Baraza la kwanza la Madiwani wa Halmashauri ya Rorya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya na Makamu wake wakiwa tayari kuendesha kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Charles Chacha (kushoto) wakishauriana jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a akifungua rasmi kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo ya wilaya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Rorya, Mara. Wa tatu kutoka kulia ni mkuu wa wilaya ya Rorya, Simon Odunga.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Rorya, Simon Odunga (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, viongozi wa Vyama vya siasa na wakidini baada ya kumalizika kwa kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya.
Baadhi ya wananchi katika Halmashauri ya wilaya ya Rorya wakifurahi jambo wakati wa kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Gerald Samwel Ng’ong’a (kulia) akipokea rasmi vitendea kazi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rorya, Charles Chacha (kushoto) kabla ya kuanza rasmi kwa Baraza la kwanza la Halmashauri hiyo.

Wananchi wakifuatilia kwa ukaribu kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a akipokea hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara Gerald Samwel Ng’ong’a akishuhudia Hakimu wa wilaya akisaini rasmi fomu zake za kiapo mara baada ya kuapa kiapo cha utiifu na kuanza kutumikia nafasi yake ya udiwani na Uenyekiti wa Halmashauri ya wilaya.
Baadhi ya jamaa wa karibu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya wakimvika mashada ya maua baada ya kukamilisha kula kiapo cha utii.
Wananchi wakifuatilia kwa ukaribu kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoani Mara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com