Mahafali yakiendelea. Wa tatu kulia waliosimama ni Mhitimu wa Shahada ya Uongozi na Rasilimali Watu, Caroline Mduma. |
Na Dotto
Mwaibale, Singida
TAASISI mahiri na kongwe ya uhasibu nchini (TIA) ipo mbioni kuanza ujenzi wa baadhi ya majengo yake kwenye kampasi yake iliyopo jiji la Mwanza, baada ya taratibu zote za michoro kukamilika.
Taasisi hiyo kwa sasa imezidi kupanua wigo wa kimafunzo sanjari na kujiimarisha katika mifumo ya utoaji elimu kuendana na teknolojia za kisasa, lengo ni kuongeza tija na kujenga uwezo kwa muhitimu kuwa mahiri na mbunifu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa Carolyne Nombo, aliyasema hayo mkoani hapa juzi, wakati akihutubia mahafali ya 18 ya Taasisi hiyo kwa Kampasi zake za Singida, Mwanza na Kigoma.
“Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Taasisi imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, maabara ya kompyuta na maktaba baada ya kufanikiwa kupata hati za viwanja vyake vilivyopo Luchelele na Nyang’homango,” alisema Prof. Nombo na kuongeza:
“Pia taasisi imetenga kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili ya ujenzi wa kantini na nyumba za watumishi katika eneo lake la Nyang’homango wilaya ya Misungwi na michoro imekamilika.”
Alisema kwa upande wa kampasi yake ya Kigoma TIA kwa mwaka huo huo wa fedha 2020/2021 imetenga shilingi milioni 450 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la taaluma, baada ya kufanikiwa kununua eneo lililopo Kamara ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Nombo alisema kwa upande wa kampasi ya Singida tayari wamekamilisha jengo la Maabara ya kisasa ya Kompyuta na Maktaba zenye uwezo wa kuhudumia wanachuo 200 kwa wakati mmoja.
Alibainisha kwamba kwa mwaka wa fedha 2020/21 taasisi hiyo imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Taaluma na uzio kwenye jengo la chuo chake kwa kampasi ya Singida.
“Mafanikio yote haya yanatokana na utendaji mzuri wa serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Jemedari Rais John Magufuli ambaye wakati wote amekuwa akitoa kipaumbele katika sekta ya elimu,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa TIA huku akisisitiza:
“Azma yetu ni kuhakikisha tunauhisha mitaala iliyopo ili iendane na mahitaji ya soko. Lengo ni kuendelea kutoa wahitimu wenye stadi stahiki za kumudu kufanya kazi mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri.”
Awali, Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga, ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa mahafali hayo, alisema serikali ipo tayari kutoa kila aina ya ushirikiano ndani ya TIA na wahitimu wake, kwa kuzingatia fani zinazotolewa zina umuhimu mkubwa kwa ujenzi wa uchumi wa Taifa.
“Endeleeni kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na kubuni mbinu mpya, fani zinazotolewa TIA ni muhimu sana katika kuendesha uchumi wa taifa letu na kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma,” alisema Maganga.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo kwa niaba ya Wizara ya Fedha, alipongeza mchango wa TIA katika kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, wavuvi na vikundi vya ushirika.
“Jitihada hizi ni za muhimu sana katika lengo la Taifa la kurasimisha shughuli za wajasiriamali wadogo, na pia ni maagizo ya Rais Magufuli katika shabaha iliyopo ya kuwawezesha kupatiwa huduma muhimu ikiwemo mikopo,” alisema.
Katika
mahafali hiyo ya 18 kwa Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma, jumla ya wahitimu
2485 wamehitimu kozi za cheti cha awali, astashahada, stashahada na shahada
katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Uongozi wa Rasilimali Watu na
Usimamizi wa Biashara.
Social Plugin